Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Juni 15, 2024 Local time: 07:16

FAO: Ukame Afrika Mashariki unaongeza mfumuko wa bei za vyakula


Mkulima akihangaika kukusanya mavuno yanayovumilia ukame katika eneo la Kwale, Kenya.
Mkulima akihangaika kukusanya mavuno yanayovumilia ukame katika eneo la Kwale, Kenya.

Bei za vyakula vinavyotumika zaidi Afrika Mashariki zimeendelea kupanda kwa kasi wakati ukame umekuwa ukinyausha mazao mashambani kabla ya kufika wakati wa mavuno.

Kwa mujibu wa Mwandishi wa VOA Shirika la Chakula Duniani (FAO) limerekodi mfumuko wa bei za mahindi, uwele na nafaka nyingine katika maeneo mengi ikiwemo Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Uganda na Tanzania.

Kadhalika katika rekodi ya bei ya nafaka, maharage sasa yanagharimu asilimia 40 huko Kenya kuliko ilivyokuwa mwaka mmoja nyuma. Na mji mkuu wa Uganda, Kampala bei ya maharage na unga wa mhogo imepanda kwa asilimia 25.

Mchumi wa ngazi ya juu FAO, Mario Zappacosta mapema amesema Jumanne kuwa kaya na wafugaji wanakabiliwa na changamoto kubwa na tayari wameathiriwa na ukame huo.

Sababu kubwa iliopelekea tatizo hili la mfumuko wa bei linatokana na hali ya mazingira ya eneo hilo ambalo ni ukame uliozikumba baadhi ya sehemu za Kusini mwa Afrika Mashariki kati ya OKtoba na Disemba.

Lakini katika baadhi ya nchi tatizo la ukame limeongezeka kutokana na sababu nyingine, kama vile migogoro na vita zinazoendelea Sudan Kusini na Somalia.

Mchumi huyo ambaye ni mratibu wa taarifa za ulimwengu na mfumo wa kutoa tahadhari ametahadharisha kuwa “mfumuko huo mkubwa wa bei” unatoa ishara mbaya kuhusu usalama wa chakula.

Bei zilipanda takriban maradufu katika miezi 12 iliyopita katika masoko mengi, pamoja na bei za nafaka. Kwa hiyo kaya nyingi ambazo hazizalishi chakula chao wenyewe, wanalazimika kutafuta sokoni na bei ziko juu sana. Pia uwezo wao wa kununua chakula hicho uko chini sana.

Usalama wa chakula ulikuwa tayari umetetereka katika eneo kutokana na mvua za El Nino. FAO inasema, “hali mbaya ya hewa na mvua zisizotabirika” zilipunguza sana mavuno.

Kwa upande wa wafugaji, wao wamekabiliwa na kushuka kwa bei ya mifugo yao kufikia theluthi moja ya kile walichokuwa wanapata mwaka mmoja uliopita. Zappacosta amesema hiyo inamaanisha wana pesa kidogo ambazo hazitoshelezi kununua chakula cha kutosha.

Akitoa mfano kwa kutumia takwimu, mchumi huyo amesema mwaka moja uliopita katika baadhi ya maeneo ya Somalia, mfugaji alikuwa akiuza mbuzi anapata kiasi cha fedha kumwezesha kununua takriban kati ya kilo 110-120 za mahindi.

Hivi leo mbuzi huyo huyo anamwezesha kununua kilo 30 za mahindi. Kwa hivyo ni wazi kuwa uwezo wake wa kuilisha familia yake umepungua kwa asilimia 70- 80.

Hali hii ya mfumuko wa bei inaweza isibadilike hivi karibuni. Mchumi wa ngazi ya juu wa FAO anasema huu ni wakati wa kiangazi katika eneo la Afrika Mashariki na hakuna mvua zinazotarajiwa mpaka mwisho wa mwezi Machi au mapema Aprili. Kwa hivyo mavuno yanayotarajiwa Julai na Agosti mara nyingine yanaweza yakawa sio ya kawaida na kuongeza kuwa sehemu ya baadhi ya nchi hizo ziko kwenye hatari.

Zappacosta amesema kuwa Katika baadhi ya nchi tunajua kuna uwezekano mkubwa wa kukabiliwa na ukame, zikiwemo Somalia, Sudan Kusini ambako ukame umeongezeka kutokana na migogoro na kutokuwepo kwa amani.

XS
SM
MD
LG