Madai hayo yalitolewa na Peiter “Mudge” Zatko, mdukuzi wa kompyuta ambaye alikuwa ameajiriwa na mkurugenzi mtendaji wa zamani wa Twitter Jack Dorsey.
Kituo cha televisheni, CNN na gazeti la Washington Post zimeripoti kwanza maelezo ya malalamiko hayo Jumanne.
Waraka wa malalamiko hayo uliorekebishwa wenye kurasa 84 uliwasilishwa kwa Bunge la Marekani.
Msemaji wa Twitter ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe amesema katika taarifa kwa VOA kwamba “Madai ya Zatko hayana msingi na yana lengo la kuihujumu Twitter, wateja wake na wanahisa wake.”
Habari hizo zilizofichuliwa zinajiri huku Twitter ikijikuta kwenye mpambano wa kisheria na mkurugenzi wa kampuni ya Tesla Elon Musk, anayechukuliwa kama tajiri mkubwa duniani.
Musk alijiondoa kwenye makubaliano ya kuinunua Twitter mwezi uliopita kwa kitita cha dola bilioni 44, akiishtumu Twitter kuficha habari kuhusu idadi ya akaunti zake za kiotomatiki, zinazojulikana kama roboti.