Meya wa jiji la New York nchini Marekani Michael Bloomberg amesema itakuwa 'siku ya kusikitisha" endapo watafanikiwa kuzuia mipango ya kujenga msikiti karibu na mahali palipotokea mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 mjini Manhattan.
Bloomberg aliuambia mkutano wa waandishi wa habari Jumatatu kuwa serikali haina sababu ya kuingilia dini za watu. Alisema kuzuia ujenzi wa msikiti na kituo cha kijamii eti kwa sababu tu itakuwa karibu na mahali ambapo mashambulizi ya kigaidi yalifanyika itakuwa siku ya kusikitisha katika historia ya Marekani.
Meya Bloomberg na watu wengine wanaounga mkono ujenzi wa kituo hicho wamesema hatua hiyo itasaidia kuondoa mfarakano baina ya nchi za Magharibi na dunia ya kiislamu.
Wapinzani kutoka chama cha Republican wamemlaumu Rais Obama kwa matamshi aliyotoa kuunga mkono haki watu wanaotaka kujenga msikiti na kituo hicho cha kijamii.