Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 10, 2023 Local time: 16:47

Mdundiko: Ngoma yenye jazba


Ngoma ya mdundiko inayopendwa katika jiji la Dar es Salaam inapendwa kutokana na jazba na timbwili timbwili zake.

NGOMA ya mdundiko ambayo ni ya wenyeji wa eneo la mji mkuu wa biashara wa dar es Salaam nchini Tanzania pamoja na maeneo ya jirani imekuwa moja ya ngoma maarufu sana katika sherehe nchini Tanzania. Kulingana na simulizi za wazee wa kabila la Kizaramo ambao ndio wenyeji wa jiji la Dar es Salaam, ngoma ya mdundiko ni ishara ya furaha na ufahari yenye chereko chereko na timbwili timbwili za kila aina. Ngoma ya mdundiko wakati wote inachezwa kwa mfumo wa kuhama hama, yaani wapigaji hufunga safari kutoka sehemu moja hadi nyingine bila kujali umbali.

Kutokana na hali hiyo si ajabu ukaona kwamba ngoma hii ikiwa imekusanya kundi kubwa la watu, wengi wakiwa wamejiunga njiani – wakiacha shughuli zao kwa muda na kujiunga na mdundiko kwa mitaa kadhaa, kabla ya kurudi kwenye shughuli zao.

Mohamed Kizaro – mkazi wa Dar es Salaam – anasema, “…ngoma ya mdundiko ni ngoma ya siku nyingi sana. Ngoma ya mababu, mabibi, na ngoma hii hasa shughuli yake kubwa ni siku ya mtoto wa kiume amefanyiwa jando, na amepona anatoka, na pia mtoto wa kike anapopata balehe au akitaka kuolewa. Kwa hiyo hasa inakuwa ngoma ya kumtambulisha yule kijana kwa ndugu – mashangazi, wajomba, bibi.

“Kwa hiyo wanazunguka jiji zima – kwenda nyumba hadi nyumba, wanaweza wakatoka Manzese kwenda Buguruni, wakatoka Buguruni kwenda Ukonga, hadi Ilala, Temeke, Mbagala, na yote hayo ni kutambulisha sasa tunamcheza mwanetu.”

Kutokana na kuzunguka kwake mjini ngoma hii imelaumiwa pia kwa kusababisha watoto kupotea, pale wanapojiunga na ngoma ikiwa katika mwendo na hatimaye kujishtukia wapo katika mtaa ambayo hawaujui na hawajui vipi kurudi nyumbani.

Zinazohusiana

XS
SM
MD
LG