Na wakati huu ambapo serikali ya mpito ya Sudan inafanya juhudi kuelekea kupatikana kwa demokrasia, kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa, wanawake wanachukuwa tena jukumu muhimu kutafuta haki na usawa.
Wanawake wa Sudan walisaidia kuandaa maandamano ambayo yalifanikisha kumuondoa madarakani rais wa muda mrefu Omar al-Bashir, hapo mwaka 2019, baada ya kukaa madarakani kwa miongo mitatu akiendesha nchi ki-imla.
Tangu kuondoka kwake wanawake wamekuwa na jukumu kubwa katika serikali mpya ya mpito.
Mwanamke ameshachaguliwa kuwa Mwanasheria Mkuu, akiwa ni wa kwanza, na si tu katika taifa la Sudan, bali pia katika ulimwengu mzima wa mataifa ya kiarabu.
Na kwa mara ya kwanza kabisa wanawake wanne nao pia wamechaguliwa kuwa sehemu ya baraza la mawaziri katika serikali mpya, ikijumuisha Waziri wa Mambo ya Nje wa kwanza mwanamke wa taifa hilo, Asma Mohamed Abdalla.
Lakini wanawake bado wanaandamana kutaka kubadilishwa kwa sheria, na kurejeshwa kwa haki zao zilizo ondolewa wakati sheria ya Kiislamu zikitumika katika utawala wa Bashir.
Chama cha wataalamu wa Sudan, SPA, kilikuwa moja ya makundi makubwa yaliokuwa nyuma ya maandamano yaliyo mwondoa madarakani rais Bashir.
Samahir Elmubarak, ambaye anaongoza tawi la SPA, chama cha wafamasia kinaendelea kuwa katika mchakato wa kisiasa.
Elmubarak : "Sijapata kuhisi tumefikia kiwango ambacho inabidi tuawaache harakati zetu. Kwa hiyo motisha kilichowapa nguvu watu kuuondoa utawala wa Bashir, ni motisha hiyohiyo ambayo inawasukuma watu kuendelea kufanikisha malengo ya mapinduzi ya kuleta uhuru, amani, na haki."
Wakati maafisa wa usalama walipokuwa wanazima maandamano ya June 3 kutetea demokrasia, zaidi ya watu 120 waliuwawa akiwemo kijana mkubwa wa Amira Kabous.
Kifo chake hakijamzuia Kabous kujihusisha na juhudi za kuleta mageuzi na hivi sasa ni naibu mkuu wa chama cha watu walopoteza jamaa zao wakati wa maandamano hayo.
Kabous anaeleza : "Kile tunachokifanya ni kuendeleza jukumu la mashuja na kujitoa mhanga Maisha yao. Bado hatujafikia malengo yetu, hatujashuhudia uhuru amani na haki mashuja walodai. Tutaendelea hadi tufanikiwe kufikia malengo yote ya mapinduzi, ambayo Watoto wetu walijitoa mhanga kupigania na kudumisha tena haki hadi tuione sudan jinsi Watoto wetu waliota kuiona.
Kabous, na Elmubarak hivi karibuni walipewa tuzo ya uhuru ya mwaka 2020 ya taasisi ya Freedom House ya hapa Marekani kwa juhudi zao za kuleta mabadiliko ya kidemokrasia Sudan. Tuzo hiyo ilitolewa chini ya ujumbe wa “nguvu ya kuandamana.”