Wizara ya ulinzi ya Russia imesema ndege zake nyingi zimeondoka Syria Jumatano, zikiendelea kuondoka wakati Umoja wa Mataifa ikisimamia mazungumzo zaidi ya amani yasiyo ya moja kwa moja huko Geneva kati ya pande zinazohasimiana nchini Syria.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anapanga kusafiri kwenda Moscow wiki ijayo kwa mazungumzo na Rais wa Russia Vladimir Putin kuhusu kupunguza wanajeshi wake huko Syria na shinikizo jipya kwa ajili ya amani katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita.
Kerry amesema atazungumza na wote - Bwana Putin na waziri wa mambo ya nje wa Russia, Sergei Lavrov - kuhusu namna ya kusonga mbele na utaratibu wa kuleta suluhisho la kisiasa kwenye taifa hilo linalokumbwa na vita kwa miaka mitano sasa.