Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Juni 22, 2024 Local time: 16:11

Mawaziri wa Kenya wahitilafiana juu ya kualikwa Bashir


Rais Omar Hassan al-Bashir apunga mkono akiwasili Kenya kuhudhuria sherehe za kutiwa saini katiba mpya mjini Nairobi
Rais Omar Hassan al-Bashir apunga mkono akiwasili Kenya kuhudhuria sherehe za kutiwa saini katiba mpya mjini Nairobi

Serikali ya Kenya inahitilafiana kutokana na kualikwa kwa rais wa Sudan, Omar al- Bashir kwenye sherehe za kuzindua katiba mpya, wakati jumuia ya kimataifa inakosoa hatua hiyo.

Wakizungumza kwenye mkutano na waandishi habari Jumapili baadhi ya mawaziri wa serikali ya Kenya walitetea uwamuzi wakumalika kiongozi wa Sudan Omar al-Bashir kwenye sherehe za kutia saini katiba mpya ya nchi hiyo. Mahakama ya uhalifu wa kimataifa ICC imeshatoa hati mbili za kukamatwa Bw. Bashir kwa tuhuma za uhalifu wa vita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauwaji ya halaiki huko Darfur.

Kenya ambayo ni mojawapo ya nchi zilzotia saini kuundwa kwa mahakama hiyo, imekosolewa vikali na jumuia ya kimataifa kwa kutomkamata rais al-Bashir na kumfikisha huko the Hague. Lakini waziri wa uchukuzi wa Kenya Amos Kimunya alieleza majukumu ya Kenya chini ya mahakama, sio mambo pekee yanayoangaliwa katika maslahi ya sera za nchi hiyo kuhusiana na Sudan.

“Maslahi ya nchi yanatangulia, maslahi ya kikanda ni ya pili. Maslahi ya kikanda ni pamoja na uwanachama wetu katika IGAD, COMESA ambapo sisi ni wanachama pamoja na Sudan na Umoja wa Afrika, ambako tunawajibika kama vile Umoja wa Afrika kutokana na maamuzi ya Umoja huo,” alisema Bw. Kimunya.

Kimunya alikua anazungumzia uwamuzi wa mwaka jana ulochukuliwa na Umoja wa Afrika AU, kupuuzi hati za kukamatwa Bw. Bashir. Uwamuzi ulichukuliwa baada ya Baraza la Usalama kupuuzi ombi la AU kuchelewesha utekelezaji wa hati hiyo kwa mwaka mmoja zaidi kwa maslahi ya amani.

Lakini akizungumza na Sauti ya Amerika waziri mkuu Raila Odinga amesema haikua jambo la busara kumualika rais Bashir katika sherehe za kuidhinisha katiba.
“Unafahamu, nimeshasema kwamba rais Bashir anahitaji kujibu uhalifu ulotendwa chini ya uwongozi wake, na ni baada tu ya kufutiwa hatia zote na ICC ndipo aruhusiwe kuhudhuria mikutano yote ya viongozi wa Afrika na mikutano mingine. Kwa hivyo msimamo wangu haujabadilika," alisema Bw. Odinga.

Serikali ya Obama imeleza kusikitishwa na hatua ya Kenya kumualika al-Bashir kwa kukaidi hati ya kukamatwa iliyotolewa na ICC.

XS
SM
MD
LG