Baadhi ya wapiga kura waliiambia Sauti ya Amerika kuwa matumizi ya kompyuta yalisababisha changamoto kwa baadhi ya wapiga kura wengi wao wakisema hawajui na hawajawahi kutumia kompyuta tangu wazaliwe.
“Mashine imeharibika, hatujui kinachoendelea hapa” alisema mwanamke mmoja aliyejitokeza kupiga kura.
Wakati huo huo wakaazi wa baadhi ya mikoa wenye hasira wamezivunja kompyuta za Tume huru ya uchaguzi.
Ombeni Muntukone ni miongoni mwa watu waliofanikiwa kupiga kura huko Bukavu amesema baadhi ya wapigakura wametumia muda mrefu ndani ya vituo vya kupigia kura.
“Namaliza kupiga kura ili kubadili mambo. Mbele ya mashine nimefanya dakika 5 ila kuna wanaomaliza dakika 10. Ikiwa mtu mmoja anamaliza dakika 5 yaani watafanya siku 2 bila kumaliza hawa watu,” alisema Muntukone.
Changamoto nyingine zilizoelezewa na wapigakura katika maeneo mbalimbali ni pamoja na baadhi ya majina ya wapiga kura huko Bukavu kutokuwepo katika orodha ya wapiga kura na kutowasili kwa vifaa vya kupigia kura katika baadhi maeneo hususani ya vijijini.
Wamesema kutowasili kwa vifaa vivyo kunatokana na ubovu wa barabara na hofu ya ukosefu wa usalama.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa Umoja wa Mataifa umekubali kutoa msada ya kusafirisha vifaa vya kupigia kura kwa ajili ya Uchaguzi wa DRC uliofanyika siku ya Jumatano, lakini haikupokea maelekezo kutoka katika mamlaka za uchaguzi kuhusu mahali ambapo vifaa hivyo vinatakiwa vipelekwe, kulingana na barua iliyoonekana na Shirika hilo la AFP.
Na pia Umoja wa Mataifa umesema Tume ya Uchaguzi haikuiarifu UN kuhusu kiwango cha vifaa vinavyohitajika kusambazwa katika majimbo hayo, miongoni mwa masuala mengine.
Kuhusu malalamiko ya kutofuatwa kwa taratibu za uchaguzi katika wilaya ya Shabunda. Agnes Sadiki, mmoja wa wanawake mashuhuri na mkazi wa wilaya hiyo ya Shabunda alisema
“Kinachoshangaza na kunikera ni kwamba nimekuta watu, wanaume wawakilishi wa wapiga kura wakigawa pesa kwa wapiga kura ndani ya kituo cha kupigia kura ili waende kuwapigia kura. Imenikera sana na kinyume cha sheria,” alisema Sadiki.
Forum