Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 24, 2024 Local time: 22:52

Mateso wanayopitia wakimbizi wa DRC kutokana na vita vya waasi


Wakimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo baada ya kuwasili katika kambi ya Kyangwali, Uganda, Feb. 16, 2018. PICHA: AFP
Wakimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo baada ya kuwasili katika kambi ya Kyangwali, Uganda, Feb. 16, 2018. PICHA: AFP

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, imekumbwa na mgogoro wa vita tangu mwaka 1996

Zaidi ya makundi ya wapiganaji au ya waasi 100 yanapigana na wanajeshi wa serikali nchini humo na yamepelekea Zaidi ya watu milioni mbili kuwa wakimbizi nje au ndani ya DRC.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, DRC ina jumla ya watu milioni 95. Nchi hiyo ina wanajeshi karibu 160,000 pekee. Athari za mapigano kati ya makundi ya waasi na wanajeshi walio wachache, zinadhihirika kati ya wananchi. Kando na kuwa na utajiri mkubwa wa madini Afrika, zaidi ya raia milioni mbili wa DRC wanaishi kama wakimbizi.

Wengi wao, wameishi maisha ya kukimbia kutoka kambi moja hadi nyingine. milio ya risasi, mizinga na mabomu imezingira maisha yao.

Dansira Karikumutima ana umri wa miaka 52. Ana watoto 11, ameishi maisha ya ukimbizi tangu alipokuwa na watoto wanne. Kwa sasa anaishi katika kambi ya Rutchuru.

“Ya kwanza na ndio nilikuwa nimezala mara ya nne, nilikimbilia Uganda. Mara ya pili tulikimbilia hapa Rutshuru. Mara ya tatu tulikimbilia kwa milima ya kinoni, na sasa tumekimbilia hapa.” Dansira amemwaambia mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya VOA.

Ajua Mungu Makeke ni mkimbizi katika kambi ya Mubimbi Kalehe.

“Waasi walikuwa wanatuvamia kila siku. Walikuwa wanatupiga na kuiba kila kitu hasa chakula. Wanabeba hata kuku. Maisha hapa ni magumu kabisa. Ni kujikaza tu. Ni kulima kwa mashamba ya watu kila siku ndipo upewe chakula.”

Hakuna msaada kwa wakimbizi wanaoishi ndani ya DRC

Asilimia kubwa ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaishi Uganda, Tanzania, Kenya na Afrika Kusini.

Kambini, matatizo ni mengi lakini zaidi ni ukosefu wa chakula.

Hakuna chakula tunapata. Nakumbuka wakati tulikuwa Uganda kambi ya Nyakabande, kwa miezi 4, tulikuwa tunakula mzuri, walikuwa wanatuletea unga, mchele, maharagwe, walikuwa wanatupikia na tunakula vizuri. Watoto walikuwa wanakunywa uji asubuhi na jioni. Hapa, hakuna kitu wanatupatia. Watu wanaoishi karibu hapa na kambi ndio walitupatia msaada wa mchele wakati tulifika na sio wote walipata. Haikuwa inatosha watoto. Njaa hapa inatupiga sana.” Amesema Dansira.

Wakimbizi wanafanya kazi kwa mashamba ya watu wanaoishi karibu na kambi

Ndani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Muungano wa makanisa ya kiroho ECC, zaidi ya 60 yanatoa msaada wa chakula kwa wakimbizi wanaoshi katika kambi. Msaada huo wa unga wa kutengeneza sima, maharagwe, mafuta ya kupika na chumvi, unatolewa kwa kila familia, mara mbili kwa mwaka. Wakimbizi wanalazimika kulima kwa mashamba watu wanaoishi karibu na kambi ili kupata msaada wa chakula.

“Kwanza mimi nguvu zinaishia. Siwezi tena kwenda kufanyia watu kazi ya kilimo kwa mashamba ya watu hapa Rutshuru. Walio na nguvu wanaenda kwa mashamba kulima au waende kuomba uomba. Chochote wanachopata, wanapikia watoto. Mimi sina nguvu, wanawatuma watoto wanaenda kuomba uomba.” Ameendelea kusema Dansira.

Wanapolazimika kulimia watu wa mashambani au watumie watoto wao kama omba omba, wanakariri kwamba waliacha chakula kingi sana katika mashamba yao na hawakuwa wanakosa hata mlo mmoja kwa siku.

Eugene Endebwami ni kiongozi wa wakimbizi katika kambi ya Rutshuru, DRC.

“Milipuko ya risasi kwenye ziko kulikuwa mavuno, huwa tunalima, tunafuga mifugo. Mimea ilikuwa imekomaa, mavuno yote imekuliwa na wale waasi wanaopigana huko. Tunaomba serikali itafute Amani na waturushidhe kwetu. Tunateseka sana.”amesema Eugene.

Mumbere Kapalata alikimbia vita vya Mai Mai. Ana umri wa miaka 31. Ana watoto sita. Ameishi katika kambi ya Minova kwa mda wa miaka 10. Wenzake wamejaribu kurudi nyumbani lakini huwa wanarudi kambini kutokana na mapigano ya waasi.

“Hapa tunaishi vibaya. Nakusanya mawe ndipo niuze nipate chakule. Tunapokea msaada wa chakula kutoka kwa kanisa mara mbili kwa mwaka. Hakitoshi kabisa. Nalimia watu shambani kutoka asubuhi hadi jioni ndipo wanipe chakula. Nina watoto sita. Nataka tu serikali itusaidie. Haya maisha tunayoishi ni magumu sana.”

Hakuna msaada wowote wanaopata kutoka kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wala kwa shsirika lolote la kutoa msaada isipokuwa muungano wa makanisa.

“Ulimwengu umetusahau licha ya kujua tunateseka”

Wanasema wamesahaulika licha ya ulimwengu kujua kwamba vita vya DRC vimesababisha mamilioni ya watu kutoroka makwao na kwamba wanaozungumziwa zaidi ni wale walio katika nchi jirani na katika kambi kubwa kubwa za wakimbizi zinazosimamiwa na shirika la umoja wa mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR.

Ndebwami Eugene ni mkuu wa kambi ya wakimbizi ya Rutshuru amabpo wanaishi katika madarasa ya shule ya msingi ya Rutshuru.

“Ni mateso juu ya mateso kwetu katika nchi hii. Wanaokimbilia nje ya nchi pia wanakumabana na mateso Zaidi. Watoto kuzaliwa kule, ni watoto. Siwezi kusema kama ni waganda ama wakongomani mi sijui. sijui hawa wakuu wetu wa nchi ya Congo wanawaza nini kuhusu wakimbizi wenzetu wako huko kwa mashida mbalimbali.”

Wakimbizi wanaishi katika madarasa, shuleni

Katika kambi ya Rutshuru, wakimbizi wanaishi katika madarasa. Walikuja hapa mwezi March mwaka huu, kutokana na vita kati ya kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa DRC mashariki mwa Congo. Wanaishi kwa madarasa ambayo ni lazima wawe wameamka alfajiri kabla ya wanafunzi kuwasili shuleni kwa masomo.

“Matatizo makubwa ni hii ya kulala nje. Tunaamka asubuhi na mapema na kutoa vitu nje ili watoto wakutoka hii jamii iliyo karibu na kambi waseome. Vitu tunaviweka nje. Vitu vinanyeshewa na mvua. wakati tunapika chakula kinanyeshewa.” Amesema Dansira.

Licha ya kuishi shuleni, watoto wao hawapati fursa ya kusoma kwa sababu hawawezi kulipa karo. Hawapati huduma ya matibabu kando na kutibiwa malaria na kupewa dawa za kupunguza maumivu.

“Matibabu hapa ni shida tupu. Afisa wa afya wa hapa alikuja na kusema kwamba tunaishi katika hatari kubwa sana. Katika hospitali ya hapa karibu, wanatibu malaria pekee yake lakini tuna magonjwa mbalimbali ambayo imetufikia.” Amesema Eugene.

Wakaimbizi wanatamani kurudi kwao

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yanasema kwamba kuzuia wimbi la wakimbizi ni swala gumu lakini la muhimu kwa sasa ni kutafuta namna wanajeshi wa DRC wanaweza kusaidiwa kurejesha Amani masharimi kwa DRC.

Jua linapochomoza, linapotua na giza kutawala saa za usiku, siku zote, wakimbizi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wana ombi moja…

“Tunachohitaji, sio kusema chakula, sio kusema mavazi. Tunahitaji Amani. Tunataka amani tu.” Amesema kiongoni wa wakimbizi wa Rutshuru Eugene Endebwami.

Idadi kubwa ya wakimbizi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wanatoka mashariki mwa nchi hiyo ambapo kundi la waasi la Allied democratic forces ADF, limetajwa kila mara kuongoza makundi mengine zaidi ya 100 kwa mauaji, kuteka watu nyara na kupelekea mamilioni ya watu kutoroka makwao na kuishi kama wakimbizi.

Makundi mengine ambayo yametajwa ni Mai mai, Codeco, Interahamwe, FDLR na M23. Yote yanadai kupigania haki za raia, kulinda raslimali za nchi, kutetea demokrasia na haki za kibinadamu.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC kwa ushirikiano na Austere Malivika na Mitima Delachance, DRC.

XS
SM
MD
LG