Makaburi ya halaiki yamepatikana karibu na Jiji kuu la Burundi la Bujumbura licha ya Serikali kukanusha kuwepo kwa makaburi kama hayo katika siku za karibuni. Taarifa ya kupatikana kwa makaburi hayo inasemekana kutolewa na kijana aliedai kujitenga kutoka kwa kundi la wapiganaji kulingana na Idara ya Polisi.
Mwisho wa mwezi Januari, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitoa madai ya kuwepo kwa makaburi ya aina hiyo likidai vyombo vya usalama huenda vilihusika, jambo ambalo Serikali imekanusha vikali.
Hali ya kiusalama imeendelea kuzorota nchini Burundi tangu Rais Pierre Nkurunziza alipotangazwa kuwa mgombea wa Urais kwa mhula mwingine na hatimae kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu uliopita licha ya uchaguzi huo kususiwa na baadhi ya vyama vya Upinzani..