Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Julai 18, 2024 Local time: 16:54

Mashirika ya kibinadamu yanataka Tanzania kusitisha shughuli ya kuwahamisha Wamaasai


Wamaasai katika mojawapo ya shughuli za utamaduni wao. PICHA: REUTERS
Wamaasai katika mojawapo ya shughuli za utamaduni wao. PICHA: REUTERS

Watetezi wa haki za kiraia na mawakili wa jamii ya wamaasai, wanaendelea kuishinkiza serikali ya Tanzania kuachana na mpango wa kuwafurusha maelfu ya wamaasai ambao ni wafugaji wa kuhama hama, kutoka kwenye ardhi yao ya asili mashariki mwa mbuga ya kitaifa ya Serengeti.

Wiki iliyopita, makabiliano makali yalitokea baada ya maafisa wa serikali wa kuchora mipaka na maafisa wa polisi walipoanza kuweka mipaka kwenye ardhi yenye ukubwa wa kilomita 1500 za mraba, ambayo serikali ya Tanzania inaripotiwa kwamba inapanga kuwapa wawekezaji kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa ajili ya utalii wa kuwinda kwa sababu za kibiashara.

Sehemu hiyo ndiyo njia wanayotumia wanyama wakati wa msimu wa kuhama hama.

Makabiliano hayo ya JunI tarehe 10 yalitokea Loliondo, ambayo ni sehemu ya hifadhi ya Ngorongoro.

Video kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha wamaasai wakiwa wamekusanyika kupinga shughuli ya kuweka mpaka.

Polisi wa Tanzania walitumia gesi ya kutoa machozi na risasi kuwatawanya wamaasai hao ambao kwa kawaida, huwa wanatembea wakiwa wamebeba mikuki na mishale.

Serikali ya Tanzania imesema kwamba afisa mmoja wa polisi aliuawa.

Takriban wamaasai 31 - wanaume 18 na wanawake 13 – wametibiwa majeraha ya risasi katika hospitali ya Narok, kwenye nchi jirani ya Kenya, Dr. Catherine Nyambura, ameambia VOA.

Watetezi wa haki za kibinadamu

Ofisi ya umoja wa mataifa inayoshughulikia haki za kibinadamu imeonya kwamba hatua ya serikali ya Tanzania ya kuweka mpaka itasababisha vurugu Zaidi. “kuweka mpaka ina maana kwamba wamaasai wataondolewa katika vijiji vya Ololosokwan, Oloirien, Kirtalo na Arash, na kuwafurusha karibu watu 70,000,” imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Ofisi hiyo imesema kwamba “imesikitihwa sana” na ripoti za matumizi ya risasi za moto na “kuna hatari kubwa sana ya maisha iwapo shughuli ya kuwaondoa wamaasai itaendelea, bila kuzingatia uwazi na kuwashirikisha watu wa jamii ya Maasa katika kufanya maamuzi.”

Umoja wa Mataifa umesema kwamba hatua ya serikali ilifuatia mkutano wa maafisa wa serikali iliyofanyika katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha, ulioamua kuanza kuwekwa kwa mipaka hiyo.

Mgogoro huo umetokea siku chache kabla ya mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoa maamuzi yake tarehe 22 mwezi Juni, kuhusu hatua ya serikali ya Tanzania kutaka kuwaondoa wamaasai katika sehemu hiyo. Mahakama hiyo yenye makao yake Arusha, Tanzania, ilitoa amri mwaka 2018, ya kuitaka serikali ya Tanzania kusitisha mpango wa kuwaondoa wamaasai katika sehemu za Loliondo na Ngorongoro.

Onesmo Olengurumwa, Mkurugenzi wa muungano wa mashirika ya kutetea haki za binadamu Tanzania, amesema kwamba hatua ya kuwaondoa wamaasai, inalenga kutoa fursa kwa kampuni ya Otterlo kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, kuwekeza katika utalii na uwindaji katika sehemu hiyo.

“Serikali ilikosea tangu mwanzoni,” amesema Olengurumwa. Ingefanya mazungumzo na watu wa sehemu hiyo na kufikia makubaliano na hata kuandikishana kwamba tunaweka mipaka, lakini lakini hatuchukui ardhi yenu. Tunaweka tu mpaka. Kama hilo lingefanyika, jamii hiyo isingekuwa na wasiwasi wala kufanya maandamano.”

Serikali yatetea hatua yake

Serikali ya Tanzania imesema kwamba inaamini sehemu hiyo ina idadi kubwa ya watu na mifugo, na kupelekea uharibifu wa mazingira.

Mwaka 2019, kabla ya janga la virusi vya Covid-19, utalii ndio ulikuwa unaongoza kwa mapato ya Tanzania, kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia.

Katika mahojiano ya radio katika kipindi cha sauti ya Amerika cha ‘kwa Undani’ msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa amesema kwamba “mimi sina taarifa yoyote kuhusu kuwepo kwa hiyo amri

lakini hakuna zuio lolote lililofanywa dhidi ya serikali kuendelea kufanya shughuli za uhifadhi. Kinachofanyika Loliondo kuweka alama ni moja ya majukumu ya kuhifadhi na halijafanyika Loliondo pekee.”

“Tunawaonyesha watu eneo wanalotakiwa kutumia na eneo lililohifadhiwa. Umuhimu wa eneo la kilomita za mraba 1500 lililopo pale Loliondo ni kubwa na lina maslahi mapana ya taifa. Pale ndipo kuna vyanzo vya maji vinavyohudumia hifadhi zetu nyingi.” Ameeleza Msigwa.

Kufuatia mgogoro huo, wakaazi na shirika la kutetea haki za binadamu la Survival International wameripoti kwamba polisi wamekuwa wakiwakamata watu wanaodaiwa kushiriki katika mgogoro huo. Taarifa ya Survival International imesema kwamba polisi walimpiga mwanamme mwenye umri wa miaka 90 baada ya kijana wake kurekodi video ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Msigwa amesema “haya maneno yanayozunguka kwenye mitandao ya kijamii, kama serikali yametusikitisha sana. Leo hii kama kuna mtu ana uthibitisho wa kuwepo majeruhi atuonyeshe. Hii maneno ya kusema wapo nchi jirani, ukishakwenda kwenye nchi nyingine kuna utaratibu wake na sheria zake na sisi kama serikali tuna mipaka ya kutoa huduma zetu kwa watu ndani ya mipaka yetu. Hatuwezi kutoka hapa na magari kwenda kwenye nchi nyingine. Hatufanyi hivyo.”

Ameongezea kusema, “tunatambua kwamba kuna makundi ya watu wachache ambao wanajaribu kuwashinkiza wananchi waone kama wanaonewa, wajaribu kufanya fujo. Sisi tunawatafuta watu wa namna hiyo, tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa sababu nchi yetu inazo sheria na hili eneo lipo kwa mujibu wa sheria.”

Wamaasai wamekimbilia Kenya

Wamaasai wengi wa Tanzania wamekimbilia Kenya, wanapopata matibabu na msaada mwingine.

Patrick Ole Ntutu, kiongozi wa jamii ya wamaasai, amesema kwamba watu wake hawatambui mpaka katika ardhi yao. “Mpaka kati ya Kenya na Tanzania uliwekwa na mkoloni. Hatuutambui,” ameiambia VOA.

Wakati huo huo, wakili wa jamii ya wamaasai Martin Ole Kamwaro amesema kwamba wanatayarisha kesi dhidi ya serikali ya Tanzania, kuifikisha katika mahakama ya usuluhisho ya kimataifa ICJ, mjini Hague.

“Hatutavumilia unyanyasaji huu, Tunaishitaki serikali ya Tanzania kwa unyanyasaji wa haki za kibinadamu.” Amesema Kamwaro.

Balozi wa Marekani nchini Taznania Donald J. Wright, aliandika ujumbe wa Twitter kwamba alifanya mazungumzo na waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa na swala kuhusu mgogoro wa Loliondo lilikuwa sehemu ya mazungumzo yao. “Nimemuomba

waziri mkuu kushirkiana na wadau kupata suluhu kwa njia ya Amani,” ameandika Wright.

Makundi kadhaa ya kutetea haki za binadamu yameishutumu serikali ya Tanzania kwa kutaka kuwaondoa wamaasai sehemu za Loliondo na Ngorongoro, na kutaka mpango huo kusitishwa mara moja.

Amnesty International imeandika “hatua hiyo ni kinyume cha sheria, inashitua kwa kiwango kikubwa na ni ukatili.”

Ripoti hii imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC. Ripoti Zaidi na Idd Uwesu akiwa Dar-es-salaam, Tanzania, na Hubbah Abdi, Nairobi, Kenya.

XS
SM
MD
LG