Maafisa wa mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa wametanagza Alhamis kwamba wajumbe wa mataifa fadhili watakutana mwezi ujao kwa mkutano wenye lengo la kuchangisha takribani dola bilioni 1.7 kwa kazi za huduma za dharura nchini Kongo. Makadirio ya msaada unaohitajika umeongezeka marudufu tangu mwaka 2017 ikimulika kuongezeka kwa matatizo katika taifa hilo kubwa la Afrika ya kati
Naibu Mratibu wa huduma za dharura wa Umoja wa Mataifa, Julien Hameis, alisema wanaanda mkutano wa kimataifa April 13 huko Geneva wenye lengo la kuhamasisha uchangishaji fedha kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC kwa mwaka 2018 lakini pia kwa miaka ijayo. Alisema baada ya wiki sita za kutembelea maeneo yaliyokumbwa na mgogoro ni kwamba wanakabiliwa na dharura na matatizo ambayo yanaathiri moja kwa moja wananchi. Mkutano huo hautazingatia katika kuchangisha fedha pekee lakini pia msaada wa kiufundi.
Kulingana na tovuti ya kitaalamu Devex ambayo inaripoti juu ya masuala ya maendeleo mkutano huo wa kutoa ahadi unafadhiliwa kwa ushirikiano wa kamisheni ya ulaya, Umoja wa Mataifa na serikali ya Uholanzi.
Januari 17 taasisi ya kimataifa inayohusika na masuala ya wahamiaji-IOM ilitambua kuna haja ya kupatikana dola bilioni 1.68 kwa ajili ya mahitaji ya dharura ya Kongo . Na inaonya kwamba hali imefikia kiwango cha hatari kwa janga kubwa kulipuka. Nchi hiyo ina kiasi cha watu milioni 10 wanaohitaji msaada wa dharura ambapo watu milioni 4.5 iliwabidi wakimbie nyumba zao kwa sababu ya mgogoro.
Mgogoro wa muda mrefu unadumaza uchumi wa eneo la mashariki mwa nchi mahala ambako makundi yenye silaha yanaendelea na harakati zao huko Kivu kaskazini na kusini, mikoa miwili mikubwa ambayo inapakana na Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi.
Mgogoro pia umezuka katika jimbo la kati kati la Kasai baada ya chifu wa kijadi Kamwina Nsapu aliyekua anapinga utawala wa Rais Joseph Kabila kuuwawa Septemba mwaka 2016.
Mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa, shirika la chakula duniani-WFP, shirika la kuhudumia watoto katika Umoja wa Mataifa-UNICEF na shirika la chakula na kilimo-FAO yalikadiria mwezi Januari kwamba watu milioni 3.2 huko Kasai wanakabiliwa na hali mbaya ya upungufu wa chakula.
Mwaka 2017 ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya huduma za dharura-OCHA iliomba dola milioni 812.5 kwa ajili ya msaada wa dharura kwa ajili ya Congo lakini ilipokea dola milioni 427.8 pekee, ikiwa ni karibu asilimia 47 ya mahitaji yake.