Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Oktoba 03, 2024 Local time: 23:54

Mashindano ya Olimpiki yamalizika rasmi


Fataki wakati wa kufungwa kwa mashindano ya olimpiki 2020 mjini Tokyo Japan.
Fataki wakati wa kufungwa kwa mashindano ya olimpiki 2020 mjini Tokyo Japan.

Baada ya siku kumi na sita za michuano mbalimbali, sherehe za kufungwa kwa mashindano ya olimpiki msimu wa joto ya mwaka wa 2020 zimefanyika Jumapili mjini Tokyo, Japan, licha ya kutokuwa na mashabiki ukumbini.

Rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki (IOC) Thomas Bach, alitangaza kumalizika rasmi kwa michezo hiyo.

Fataki zilijaa angani huku baadhi ya mashabiki waliokusanyika nje ya ukumbi mkubwa mjini Tokyo, wakishangilia kwa shangwe na vigelegele.

Hafla hiyo, iliyohudhuriwa na wageni wachache tu mashuhuri, na viongozi wa baraza la kimataifa la olimpiki, ilianza kwa kupeperushwa kwa bendera ya Japan katika ukumbi wenye viti 68,000, ambako mashabiki hawakuruhusiwa kwa sababu ya masharti makali yaliyowekwa, katika juhudi za kupambana na maambukizi ya Corona.

Kwa ujumla, kulikuwa na aina 33 ya michezo ambayo wanamichezo kutoka nchi mbalimbali walishiriki.

Sherehe za kufungwa kwa mashindanio ya Olimpiki 2020 mjini Tokyo, Japan.
Sherehe za kufungwa kwa mashindanio ya Olimpiki 2020 mjini Tokyo, Japan.

Marekani imeibuka mshindi kwa kuwa na medali 39 za dhahabu, ikifuatiwa kwa karibu na China iliyozoa medali 38 za dhahabu. Japan ilifuata kwa medali 27, ikifuatiwa na Uingereza, iliyozoa medali 22, huku Russia ikiwa na medali 20 za dhahabu.

Kenya ilishinda medali nne za dhahabu, huku Uganda ikipata mbili. Afrika Kusini na Ethiopia, zilipata medali moja ya dhahabu, kila mmoja.

Saa chache kabla ya hafla hiyo ya kufunga kuanza, bingwa wa mbio za marathon raia wa Kenya Eliud Kipchoge alisema "ametimiza" ndoto yake ya kuwa mwanariadha wa kwanza tangu mwaka wa1980 kuhifadhi taji la mbio za Olimpiki. Kipchoge, ni mtu wa tatu kushinda mbio za masafa marefu mtawalia katika michezo ya Olimpiki, ambapo alimaliza mbio hizo kwa muda wa saa mbili dakika nane na sekunde 38.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 36, ambaye ametambuliwa kama mkimbiaji bora zaidi, alimaliza mbio hizo mbele ya Abdi Nageeye wa Uholanzi, kwa dakika moja na sekunde 20.

Michezo ijayo ya Olimpiki ya msimu wa joto itafanyika mwaka wa 2024 mjini Paris, Ufaransa.

XS
SM
MD
LG