Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 11:18

Mashambulizi Sri Lanka: Idadi ya vifo yafikia 207


Jamaa ya mmoja wa watu waliouawa kwenye milipuko nchini Sri Lanka.
Jamaa ya mmoja wa watu waliouawa kwenye milipuko nchini Sri Lanka.

Watu saba wamekamatwa kufuatia mashambulizi ya mabomu yaliyotokea mapema Jumapili nchini Sri Lanka na kusababisha maafa na uharibifu mkubwa wa mali.

Katika mashambulizi mabaya Zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo ndani ya kipindi cha mwongo mmoja, milipuko kadhaa ilitokea kwenye makanisa na mahoteli ya kifahar na kuwaacha angalau watu 207 wakiwa wamekufa na Zaidi ya 400 kujeruhiwa.

Milipuko sita ya kwanza ambayo ilisikika mwendo wa saa mbili na dakika arobaine na tano asubuhi, ndiyo iliyoua watu wengi Zaidi.

Milipuko miwili midogo ilitokea saa kadhaa baadaye. Mabomu hayo yalilenga waumini wa kanisa katoliki waliokuwa kwenye ibada ya Pasaka, pamoja na watalii katika miji mitatu ya Sri Lanka, ikiwa ni pamoja na mji mkuu Colombo.

Mashambuzi hayo yamewashtua raia wa nchi hiyo ambayo imekuwa tulivu tangu umwagikaji mkubwa wa damu uliosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe takriban mika kumi iliyopita.

Takriban raia 30 wa kigeni, wakiwa ni pamoja na Wamarekani na Waingereza, ni kati ya waliouawa au kujeruhiwa kwenye mashambulizi hayo ya Jumapili.

Wakristo ni asili mia saba na nusu ya watu wote nchini humo, ambako idadi kubwa ni waumini wa Budha. Sri lanka ina takriban watu milioni 21.

Kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki Papa Francis aliongoza ibada ya Pasaka iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini na watalii, kwenye kanisa la St Peters Basilica, mjini Vatican, na kutuma salamu za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa waathiriwa wa mashambulizi hayo.

Papa Francis alieleza masikitiko yake kufuatia mashambulizi hayo na kuiombea jamii ya Wakristo, ambao alisema, walilengwa kwenye makanisa, pamoja na wageni waliokuwa kwenye mahoteli. Papa Francis aidha aliombea amani nchini Syria, Yemen, Libya na Sudan Kusini.

Akizungumza kwenye ukumbi wa St Peter Square uliojaa maua ya kurembesha, Papa Francis, akiwa na mavazi meupe, alitoa ujumbe wake wa Baraka kwa mji wa Vatican na ulimwengu mzima, na kabla ya maneno yake ya mwisho ya kuwatakia watu wote Pasaka Njema, alisema alipokea habari kuhusu mashambulizi ya Sri Laanaka kwa huzuni mkubwa.

Aidha kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki aliziombea nchi za Venezuela na Nicaragua, na kueleza matumaini yake kwamba mizozo inayoendelea huko itatatuliwa kwa njia ya amani.

Maadhimisho ya sikukuu ya Pasaka hufanyika kama mwisho wa wiki takatifu kwa Wakristo, ambapo kati ya mengine, Yesu alishiriki chakula cha jioni cha mwisho na wanafunzi wake siku ya Aljhamisi, kabla ya kusulubiwa siku ya Ijumaa, ijulikanayo kama Ijumaa kuu.

XS
SM
MD
LG