Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Oktoba 10, 2024 Local time: 19:57

Kenya yaanza kutekeleza sheria dhidi ya mifuko ya plastiki


Mamlaka ya kitaifa kuhusu mazingira nchini Kenya imeanzisha operesheni ya kuwasaka watumiaji au watengenezaji wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku nchini humo kuanzia mapema Jumatatu.

Maafisa kutoka mamlaka hiyo ya maarufu NEMA kwa wakati huu wanashirikiana na maafisa wa polisi kuwasaka watu wanaokiuka sheria hiyo mpya.

Serikali ya Kenya ilitoa muda wa miezi sita kwa wadau wote wakiwapo watengenezaji na watumiaji wa mifuko ya plastiki kujadili na kuhamasisha umma, ili kujiandaa kwa utekelezaji wa marufuku hiyo kuanzia Jumatatu Agosti 28.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa adhabu itakayotolewa kwa watu wanaokutwa na hatia ni pamoja na kifungo cha hadi miaka minne gerezaji au kutozwa faini ya hadi dola 40,000.

Waziri wa mazingira nchini Kenya Bi Judi Wakhungu alisema nchi nzima inahitaji mazingira safi.

“Mifuko hii ya plastiki inadhuru mazingira yetu na kuhatarisha afya za watu wengi, ni lazima kuchukua hatua zifaazo tena kwa wakati huu ambapo marufuku hii inaanza kutumika”, alisema waziri Wakhungu.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kupitia shirika linalohusika na mazingira inaonesha kuwa maduka ya Supermarket pekee nchini Kenya hutoa zaidi ya mifuko milioni 100 kila mwaka.

Na hii ndiyo mifuko inayolengwa katika marufuku hii mpya kwa sababu hutumika kwa muda mfupi kubebea bidhaa kisha hutupwa, lakini huchukua miaka mingi bila kuoza katika mazingira.

“Sasa wakipiga marufuku mifuko yote na sisi tutatumia nini kubeba na kuhifadhi taka katika nyumba zetu”, aliuliza Bi Roselyne Nabwire katika mahojiano na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika.

Wakenya wengi bado wanahitaji kutumia mifuko hii na huenda ikawachukua muda mrefu zaidi kuzoea, japo kuna wengine wengi waliokaribisha hatua ya serikali kusafisha mazingira.

Utafiti wa kisayansi wa shirika la UNEP unakadiria kuwa kutokana na kiwango kikubwa cha plastiki zinazomiminwa baharini, ifikapo mwaka 2050 huanda plastiki zikawa nyingi kuliko samaki.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Josephat Kioko, Kenya

XS
SM
MD
LG