Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 27, 2022 Local time: 22:05

Marekani yawafukuza wanadiplomasia 60 wa Rashia


Ubalozi mdogo wa Rashia huko Manhattan, New York

Serikali ya Marekani Jumatatu imeamrisha wanadiplomasia 60 wanaotuhumiwa kwa ujasusi kuondoka nchini ndani ya wiki moja.

Dazeni za washiriki wa Marekani, ikiwemo Ufaransa, Ujerumani na Poland, pia wanachukua hatua kama hiyo katika kujibu kwa pamoja shambulizi la sumu dhidi ya jasusi wa zamani wa Rashia na binti yake huko mji wa Salisbury, Uingereza.

Hatua hiyo ya Marekani, pamoja na kufunga kwa balozi ndogo za Rashia nchini, ni kujibu kitendo cha kutisha cha kukiuka kwa serikali ya Moscow mkataba wa kimataifa wa utumiaji wa silaha za kemikali,” kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje.

Uingereza na nchi kadhaa nyingine na Umoja wa Kujihami wa Ulaya (NATO) wanailaumu Rashia kwa kufanya shambulizi hilo la kemikali.

Rashia imeendelea kusikika “ikihamasisha vitendo vya ubabe na ukandamizaji,” amesema afisa wa ngazi ya juu wa Marekani, akieleza hatua hizo za White House.

Marekani pia imeagiza kufungwa ifikapo April 2, balozi ndogo ya Rashia katika mji wa Pacific port huko Seattle katika jimbo la Washington, ikieleza kuwa uko karibu na kiwanda cha kutengeneza ndege aina ya Boeing na kituo cha kijeshi cha Kitsap, ikiwa ni bandari ya jeshi la majini la Marekani la manuari zinazobeba silaha za nyuklia.

Ubalozi huo mdogo ni “sehemu ya tatizo kubwa ambalo halikubaliki la kuwepo idadi kubwa ya maafisa wa Rashia ndani ya Marekani na “tuko tayari kuchukua hatua zaidi, ikibidi,” afisa wa ngazi ya juu wa serikali amewaambia waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kutolewa tamko hilo asubuhi Jumatatu.

“Marekani imechukua hatua hii kwa kushirikiana na washirika wetu wa NATO na nchi nyingine duniani kujibu shambulizi lililofanywa na Rashia wakitumia sumu katika ardhi ya Uingereza, ikiwa ni mwendelezo wa mbinu za kudhoofisha shughuli mbalimbali duniani,” amesema msemaji wa White House Sarah Huckabee Sanders katika tamko lake.

“Marekani imesimama imara kushirikiana katika kujenga mahusiano bora zaidi na Rashia, lakini hili linaweza kufanyika kwa serikali ya Rashia kubadilisha mwenendo wake,” Huckabee Sanders ameongeza katika tamko lake.

Rais Donald Trump, ambaye aliongea na Rais wa Rashia Vladimir Putin Jumanne iliyopita, amehusishwa katika mazungumzo ya kuwafukuza wanadiplomasia hao, kwa mujibu wa maafisa wa serikali.

“Bila shaka huu ni uamuzi wake,” amesisitiza afisa wa ngazi ya juu katika mazungumzo yake Jumatatu na waandishi.

Trump alikuwa hajampigia simu Putin kumfahamisha uamuzi huu, lakini badala yake Balozi wa Rashia Anatoly Antonov amefahamishwa hilo Jumatatu asubuhi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, kwa mujibu wa afisa huyo.

Amri ya kufukuzwa itawandosha Warusi 48 katika balozi na balozi ndogo kadhaa nchini Marekani na 12 ambao wanawakilisha Moscow katika Umoja wa Mataifa, Jiji la New York ambao “wametumia vibaya haki zao za ukazi,” kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu wa Marekani.

“Hatua tulizochukua zimefuata Mkataba wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,” amesema Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley katika tamko lake.

Wote wale ambao wamefukuzwa wanakadiriwa kuwa ni majasusi ambao “wamejificha nyuma ya pazia la kinga ya kidiplomasia wakati wakijishughulisha na vitendo vya ujasusi,” kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu wa utawala wa Marekani.

Iwapo Rashia watajibu hatua hiyo kwa kuchukua hatua za kuwafukuza wanadiplomasia wa Marekani, Washington inaweza kuchukua hatua zaidi, kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu wa Marekani, akigusia kuwa dazeni ya majasusi wengine wa Rashia ambao wameruhusiwa kubakia nchini wanaweza kukabiliwa na hatua wao pia kufukuzwa.

Jasusi wa zamani Sergei Skripal nab inti yake, Yulia walikutwa wamepoteza fahamu katika benchi la kupumzika kwenye bustani moja katika mji wa Salisbury, Uingereza na kupelekwa haraka hospitali, ambapo wameendelea kutokuwa na fahamu.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May alitangaza hatua kadhaa za kulipiza kisasi dhidi ya Rashia kutokana na kutumia sumu, ikiwemo kuwafukuza wanadiplomasia 23 wa Rashia.

Moscow imekanusha kujihusisha na shambulizi hilo la sumu na imewafukuza idadi sawa ya wanadiplomasia wa Uingereza huko Moscow.

Ujerumani na Poland wamesema wameamrisha wanadiplomasia wanne wa Rashia kuondoka katika nchi hizo, wakati huko Lithuania, wanadiplomasia watatu wameamrishwa kuondoka nchini.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG