Marekani imelaani mashambulizi yaliofanywa na makundi ya watu wenye silaha katika miji ya kaskazini mwa mali.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Victoria Nuland aliwaambia waandishi wa habari kwamba Marekani ina wasi wasi kuhusu kuendelea kwa ghasia katika miji ya kaskazini mwa Mali . Aliomba kuanza tena kwa mazungumzo kuelekea usuluhishi wa amani kwa mzozo unaoendelea.
Mamia ya waandamanaji waliweka vizuizi vya barabarani na kuchoma matairi alhamisi katika mji mkuu wa Mali kufuatia mapigano kati ya majeshi ya serikali na vikosi vya waasi wa Tuareg. Waandamanaji hao walisababisha shughuli kusimama mjini Bamako wakati wakipinga serikali jinsi ilivyokabiliana na uasi ambao umekamata miji kadhaa ya kaskazini.