Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 29, 2022 Local time: 00:22

Marekani yaadhimisha 9/11


Rais Donald Trump na mkewe, Melania Trump, waadhimisha miaka kumi na minane tangu mashambulizi ya 9/11 kufanyika.

Wamarekani Jumatano waliadhimisha miaka 18 tangu kufanyika kwa mashambulizi ya tarehe 11 mwezi Septemba mwaka 2001 ambayo yalisababisha vifo vya takriban watu 3000, katika majimbo ya New York, Virginia na Pensylvania.

Rais Donald Trump alihutubia jamaa na marafiki wa waathiriwa wa mashambulizi hayo kwenye hafla iliyofanyika katika makao makuu ya kijeshi na wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, kwenye jimbo la Virginia - nje kidogo ya mji mkuu, Washington DC.

Trump alisema kuwa Marekani kamwe haitasahau mashambulizi hayo ya kigaidi.

"Katika siku nne zilizopita, tumewashambulia maadui wetu kwa njia ambayo hawajawahi kushuhudia," alisema Trump bila kufafanua.

Rais huyo, ambaye alikuwa ameandamana na mkewe, Melania Trump, aidha alisema matukio hayo ya mwaka 2001 yaliwapa ujasiri hata zaidi raia wa Marekani.

Rais wa zamani wa Marekani, George W Bush, ni kati ya viongozi walioweka shada la maua katika sehemu maalum ya kumbukumbu ya waliopoteza maisha yao siku hiyo nje ya majengo ya Pentagon. Bush ndiye aliyekuwa kiongozi wa Marekani wakati wa mashambulizi hayo.

Mjini New York, majina ya watu waliouawa wakati wa mashambulizi hayo, yalisomwa katika hafla iliyofanyika kwenye kumbukumbu na bustani maarufu kama "Ground Zero."

Makamu wa Rais, Mike Pence, aliongoza hafla iliyofanyika mjini Shanksville, Penslvania, karibu na mahali ambapo Ndege ya United Airlines, ilianguka baada ya abiria kukabiliana na magaidi waliokuwa wameiteka, wakiwa na nia ya kushambulia ikulu ya Marekani hapa mjini Washington DC.

Maeneo mengine mbalimbali ya nchi pia yaliadhimisha siku hiyo.

Maadhimisho ya 9/11 yaliyofanyika katika jimbo la Arizona.
Maadhimisho ya 9/11 yaliyofanyika katika jimbo la Arizona.

Haya yalijiri siku chache baada ya Rais Trump kutangaza kwamba alikuwa amefuta mwaliko aliokuwa ametoa kwa viongozi wa kundi la wanamgambo wa Taliban, kuzuru Marekani kwa mazungumzo ya kutafuta anmani nchini Afghanistan.

Taliban walishutumiwa kuhusika kwa njia moja au nyingine na mashambulizi hayo.

Mhadhiri wa chuo kikuu cha New York, Prof. David Monda, aliiambia Sauti ya Amerika Jumatano kwamba Marekani sasa imetambua kuwa haiwezi kutokomeza ugaidi kwa kutumia silaha za kijeshi.

Monda alisema licha ya hali ya kulinda usalama kwendelea kuimarishwa katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini Marekani, bado kuna wasiwasi kuhusu ugaidi kwingineko duniani.

“Ingawa hapa Marekani takwimu zinaonyesha kwamba ugaidi umepungua, bado kuna maeneo mengine duniani ambayo yanaendelea kuathiriwa mno na vitendo vya ugaidi,” alisema.

Aliongeza kwamba ugaidi unaotekelezwa na Wamarekani wenyewe, ni changamoto kubwa kwa utawala wa Trump.

Mashambulizi hayo yalibadilisha kabisa jinsi Marekani inavyotzazama ugaidi na usalama wa kitaifa.

Siku moja kabla ya maadhimisho hayo, mshauri wa Rais Trump wa masuala ya Uslama wa Kitaifa, John Bolton, alifutwa kazi kufuatia kile rais huyo alisema ni "kuchukua misimamo mikali juu ya masuala ya diplomasia ya kimataifa."

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG