Msemaji mpya wa Ikulu ya White House anayeingia madarakani, Sean Spicer anaendelea kupunguza matumaini kwamba rais mteule wa Marekani, Donald Trump karibuni atatoa taarifa mpya kuhusu habari kipelelezi za Marekani zilizobaini kuwa Russia ilihusika katika uhalifu wa mitandao kwa kupenya kwenye kompyuta za hasimu wa kisiasa wa Trump na kutoa taarifa zilizomfanya Trump ashinde.
"siyo suala hasa la kutoa hiyo taarifa," Spicer alikiambia kituo cha televisheni cha CNN Jumatatu. "Ataongea kuhusu majumuisho yake na anavyofikiria juu ya kadhia yote hii. Hatatoa taarifa juu ya kitu chochote kilichokusudiwa kwa nafasi yake kama rais au taarifa zilizo kuwa siri ya taifa. Nafikiri atakachofanya ni kuwashirikisha watu kufahamu majumuisho ya ripoti na vile anavyofahamu kuhusu hali hiyo na kuhakikisha kwamba watu wanaelewa kuna maswali mengi kila mahali."
Wakati huo huo rais mteule, Donald Trump ameeleza wasi wasi wake mpya katika kilele cha mwaka mpya juu ya taarifa za mwisho za kipelelezi zinazoihusisha Russia katika kuvuruga uchaguzi wa Marekani kupitia uhalifu wa mitandao.
Taarifa hizo za kipelelezi ambazo zilipelekea rais Barack Obama kuweka vikwazo kwa vyombo vya ujasusi vya Russia wiki iliyopita na kuwafukuza wanadiplomasia 35 ambao alisema ni majasusi.
Trump akiwa katika maadhimisho ya sherehe za mwaka mpya katika jumba lake la kifahari huko Florida, aliwaambia waandishi wa habari kwamba anataka vyombo vya ujasusi vya Marekani kuwa na ushahid, "kwasababu tuhuma hizo ni nzito, na nataka wawe na uhakika."
Amesema itakuwa siyo "haki" kuja na madai hayo dhidi ya Moscow ikiwa hakuna uhakika juu ya hilo.
Rais mteule ambaye zimebakia siku 18 kabla ya kuapishwa kama rais wa 45 wa Marekani, amesema anafahamu vizuri madai ya Washington dhidi ya Russia kuliko vile ilivyoelezewa na kuwa "mtajua hilo siku ya Jumanne au Jumatano."
"na pia mimi najua suala la uhalifu wa mitandao," amesema. "na pia uhalifu wa mitandao ni jambo gumu sana kuthibitisha. Kwa hivyo inawezekana ikawa mtu mwingine mwenye kuhusika na jinai hiyo. Na pia najua vitu ambavyo watu wengine hawajui, na hivyo hawana uhakika na kadhia yote hiyo."
Hivi karibuni rais wa Russia, Vladimir Putin alisema Moscow haitowafukuza wanadiplomasia wa Marekani kwa kujibu vikwazo vilivyowekwa Alhamisi na rais Barack Obama kwa tuhuma kuwa vyombo vyake vya kipelelezi viliingilia kati kuvuruga uchaguzi mkuu wa Marekani mwezi Novemba 2016.