Maporomoko ya matope yameuwa watu watu sita na wengine kadha kubanwa katika nyumba zilizovunjika katika eneo la Mathare mjini Nairobi Jumatano, maafisa wa serikali wanasema.
Jiwe kubwa inasemekana liliporomoka katika nyumba za Mathare baada ya kung'olewa na matope na kuvunja nyumba kadha mapema Jumatano kufuatia mvua kubwa. Maafisa wanasema watu kadhaa wangali wamebanwa katika nyumba.
Watu wasiopungua wanne walitolewa wakiwa hai, lakini juhudi za uokozi zilikuwa ngumu kutokana na matope na mvua zilizokuwa zikiendelea. Afisa mmoja wa shirika la Msalaba Mwekundu anasema zaidi ya nyumba 40 zilivunjwa na maporomoko hayo.
Afisa mmoja wa polisi amesema kazi za uokozi pia zinazuiliwa na ukosefu wa barabara kufikia maeneo hayo ya mabanda. Mathare ni eneo la mabanda ya watu masikini yaliyojengwa bila mpangilio maalum na hivyo kukosa huduma za kawaida za mijini.