Mapigano makali yalizuka nchini Sudani Kusini siku ya Jumatatu saa chache baada ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwapokea viongozi wa pande mbili zinazozozana kudhibiti vikosi vyao na kuonya kwamba mashambulizi dhidi ya raia na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa huenda yakachukuliwa kama uhalifu wa kivita.
Milio ya risasi na milipuko ilishuhudiwa mjini Juba kwa siku ya tano mfululizo baada ya hali kutulia kidogo Jumapili usiku. Balozi wa Japan nchini Sudan Kusini Korro Bessho ambaye ndiye rais wa sasa wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, lililo na nchi wanachama 15 alizungumza kwa niaba ya baraza hilo siku ya Jumapili mjini New York nchini Marekani baada ya mashauriano yaliyochukua zaidi ya saa tatu kuhusu mzozo huo wa Juba.
Aliitaja hali inayoendelea kuwa tete na kusema kwamba mlinda amani mmoja mwenye asili ya kichina ameuawa na wengine kadhaa kutoka Rwanda wamejeruhiwa. Ripoti za radio nchini Sudan Kusini zimesema kuwa takriban watu 276 wameuawa katika kipindi cha siku kadhaa za vita huku msemaji wa Makamu wa Rais wa kwanza wa nchi hiyo Riek Machar akisema kuwa watu wapatao 150 ndio waliouawa na wengine wengi kujeruhiwa.