Maafisa wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaripoti kwamba huwenda mamia ya watu wamefariki baada ya boti mbili kupindukia katika majimbo mawili ya nchi hiyo.
Katika tukio moja, boti ilizama Jumapili baada ya kugonga kitu ndani ya mto Ruki katika jimbo la kaskazini magharibi la Equateur. Msemaji wa serikali ya jimbo hilo anasema, watu 15 wamefariki na wengine 60 hawajapatikana bado. Anasema boti ilikua inasafiri wakati wa usiku bila ya taa.
Katika tukio jingine boti ya mizigo iliwaka moto na kupindukia katika mto Kasai huko kusini mwa Congo siku ya Jumamosi. Watu walionusurika wanasema kulikuwepo na karibu abiri 200 na ni wachache walioweza kuchupa na kuogelea hadi kwenye ufukwe.
Waziri wa Habari wa Congo Lambert Mende, ameiambia Sauti ya Amerika kwamba maafisa hawajajuia idadi ya walofariki hadi hivi sasa akisema kuna takriban watu 24 walionusurika. Bw Mende anasema katika tukio la Jumamosi moto ulianza baada ya baadhi ya mapipa ya mafuta kuwaka moto. Anasema boti hiyo ya mizigo haikua na ruhusa ya kupakiza abiria.