Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 13, 2024 Local time: 22:39

Mali: Waliokuwa waasi wa Tuareg wadai kushambuliwa na Jeshi na mamluki wa Wagner


Waasi na wapiganaji wa Mali.
Waasi na wapiganaji wa Mali.

Waliokuwa waasi wa Tuareg kaskazini mwa Mali walisema kuwa vikosi vyao vilishambuliwa siku ya Ijumaa na jeshi na kundi la mamluki la Russia, Wagner.

Kundi liitwalo the Coordination Of Azawad Movement, CMA, lilisema katika ujumbe kwenye mtandao wa Facebook kwamba vikosi vyao " vilizuia shambulio la jeshi la Mali maarufu kama FAMA, na lile la kikosi cha Wagner" katika mji wa Ber, kaskazini mwa jimbo la Timbuktu.

"Tunaita jumuiya ya kimataifa kushuhudia vitendo hivi vibaya," alisema msemaji wa CMA Mohamed Ramadane, akilaani shambulio hilo kama "ukiukaji wa ahadi na mipango yote ya usalama."

Jeshi la Mali limesema "limelipiza kisasi vikali" dhidi ya "jaribio la kuingilia" maeneo yao siku ya Ijumaa, likiwalaumu "magaidi" kwa tukio hilo.

Siku ya Alhamisi, waasi wa zamani wa Tuareg walitangaza kuondoka kwa wawakilishi wao wote kutoka Bamako, kwa sababu za "usalama", na kuongeza zaidi pengo kati yao na uongozi wa kijeshi, ambao umekuwa madarakani tangu mwaka wa 2020.

CMA ni muungano wa vikundi vinavyotawaliwa na Watuareg vinavyotafuta uhuru kutoka kwa taifa la Mali.

Ni moja ya pande zinazohusika katika makubaliano ya amani ya 2015 na serikali ya Mali.

Serikali ya kijeshi ya Mali imetofautiana na mkoloni wa zamani Ufaransa na kugeukia Russia kwa msaada wa kisiasa na kijeshi.

Kundi la Wagner linafanya shughuli zake kwa uwazi nchini Mali na angalau nchi nyingine tatu za Afrika, na kwa kawaida huimarisha serikali dhaifu, huku likipata madini na utajiri mwingine wa asili.

Nchini Mali, wanamgambo wa Wagner hulinda utawala, kuendesha shughuli za kijeshi na mafunzo, na kushauri juu ya marekebisho ya sheria za madini na hata katiba.

Utawala wa Bamako unasema wakufunzi wa kijeshi wa kigeni nchini Mali sio kutoka kwa kundi la Wagner lakini kutoka kwa jeshi la kawaida la Russia.

Forum

XS
SM
MD
LG