Hatua hiyo inatoa nafasi ya kutozingatia tena matakwa ya makundi ya kutetea demokrasia ambao yalikuwa yanagawana madaraka na jeshi hilo kabla ya mapinduzi ya mwezi Oktoba.
Kulingana na shirika la habari la Reuters, mkataba huo unatolewa wakati utawala wa kijeshi ukiwa unakabiliwa na shinkizo kubwa kutokana na hali mbaya ya uchumi na maandamano ya kila wiki licha ya msako mkali wa maafisa wa usalama.
Hatua ya jeshi kuchukua madaraka, ilichelewesha juhudi za kurejesha nchi hiyo katika hali ya utulivu na matumaini ya kurudisha Sudan katika hali ya kawaida baada ya miongo kadhaa ya mapigano na kutengwa kiuchumi baada ya kupinduliwa kwa Omar al-Bashir mwaka 2019 kupitia kwa maandamano ya raia.
Vyanzo vya habari kutoka kwa makundi yanayounga mkono mkataba huo, vimesema kwamba unaungwa mkono na baadhi ya vyama vya kisiasa vyenye uhusiano na jeshi, waliokuwa waasi waliosaini mkataba wa amani wa mwaka 2020 na baadhi ya viongozi wa kijamii na kidini.