Mkutano wa wiki moja wa makamanda wa majeshi ya ardhini kutoka barani Afrika unaendelea mjini Kampala. Lengo likiwa kudumisha amani barani Afrika hasa nchini Somalia, Nigeria na kwenye eneo la maziwa makuu. Hii ni mara ya tatu ya makamanda hawa kukutana.
Mkutano huu unafanyika wakati serikali ya Nigeria inapotafuta mbinu za kupambana na kundi la Boko Haram, Somalia ikipambana na wanamgambo wa Al-shabaab, nalo eneo la maziwa makuu likimsaka Joseph Kony kiongozi wa kundi la waasi wa LRA.
Akizungumza kwenye mkutano huu, rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema kundi la Boko Haram na lile la Al-shabaab ni makundi ya kijinga tu kwa sababu yamefilisika ki mawazo.
Akilizungumzia kundi la waasi wa LRA, rais Museveni aliilaumu Sudan kwa kuendelea kuwapa msaada waasi wa LRA.
Amesema Sudan ilifadhili ugaidi ulioongozwa na Kony, kile anachosikia watu wakiita Lords Resistance Army. Hii ndio sababu vita dhidi ya kundi hili vilichukua muda mrefu lakini mwaka wa 2003 tulilishinda kundi hili na hatimaye likakimbilia Garamba mwaka wa 2005
Msemaji wa kamati ya maswala ya kigeni kwenye bunge la Sudan Mahdi Ibrahim Mohamed anasema waliruhusu jeshi la Uganda kumsaka Kony nchini mwao. Lakini kama wangekuwa wanashirikiana naye wazingefanya hivyo.
Mkutano huu utamalizika Jumamosi.