Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Juni 16, 2024 Local time: 14:39

Majeshi ya Nigeria yashambulia kambi za Boko Haram


majeshi ya Nigeria katika harakati za kukabiliana na waasi wa Boko Haram
majeshi ya Nigeria katika harakati za kukabiliana na waasi wa Boko Haram
Majeshi ya Nigeria yamefanya mashambulizi ya anga dhidi ya makambi yaliyoshukiwa kuwa ya wanamgambo wa ki-Islam huko kaskazini-mashariki mwa nchi.

Msemaji wa serikali ya Nigeria alisema makambi kadhaa yalilengwa na mashambulizi yaliwauwa idadi kadhaa ya waasi.

Baadhi ya mashambulizi yalifanyika katika mbuga za wanyama za Sambisa katika jimbo la Borno, eneo linalojulikana la maficho ya kundi lenye msimamo mkali la Boko Haram.

Mashahidi waliripoti kuwepo kwa wanajeshi na ndege za kivita katika jimbo la Borno siku ya Jumatano siku moja baada ya Rais Goodluck Jonathan kusema kundi la Boko Haram liliteka maeneo kadhaa katika jimbo.

Rais alitangaza hali ya dharura katika jimbo la Borno na majimbo ya jirani ya Yobe na Adamawa na aliamuru majeshi ya usalama kuchukua “hatua zote muhimu dhidi ya wanamgambo”.

Kundi la Boko Haram limekuwa likipigana na serikali tangu mwaka 2009 katika juhudi za kuwepo sheria ya ki-Islam katika eneo la kaskazini mwa Nigeria linalokaliwa na waislam wengi.

Katika mkanda wa video wiki hii kiongozi wa kundi hilo alidai kundi hilo linahusika katika mashambulizi ya karibuni katika miji ya Baga na Bama na alisema wanamgambo wataanza kuwateka nyara wanawake na watoto kama sehemu ya mkakati wao.

Zaidi ya watu 3,000 wameuwawa katika ghasia zilizohusisha kundi la Boko Haram ikiwemo mamia waliouwawa katika operesheni ya serikali ya kukabiliana na waasi.
XS
SM
MD
LG