Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 06, 2022 Local time: 09:56

Majeruhi Somalia wapelekwa Uturuki kwa matibabu


Mtoto aliyejeruhiwa akisaidiwa na wauguzi kabla ya kusafirishwa kwenda Uturuki kwa ajili ya matibabu baada ya mlipuko wa bomu Mogadishu, Somalia, Disemba. 29, 2019.

Maafisa wa serikali ya Somalia wamesema Jumapili kwamba majeruhi takribani 16 walioathiriwa vibaya Jumamosi asubuhi kutokana na shambulizi la bomu ambalo liliuwa takriban watu 90 katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu wamesafirishwa kwenda Uturuki kwa matibabu.

Waziri wa Mambo ya ndani nchini Somalia, Mohamed Abukar Islow Duale aliiambia VOA kwamba ndege ya mizigo ya jeshi la Uturuki imewachukuwa majeruhi 16 kwenda Ankara kwa matibabu.

Raia wawili wa Uturuki walikuwa miongoni mwa waliokufa katika shambulizi hilo la bomu.

Ndege hiyo ya Uturuki kabla ya kuwachukua majeruhi hao ilishusha vifaa vya kitabibu pamoja na madawa kusaidia mahospitali ya Mogadishu yaliyojaa wagonjwa ili kukabiliana na idadi kubwa ya majeruhi wa sasa kutokana na shambulizi.

Wakati huo huo, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis siku ya Jumapili aliwaombea waathirika wa shambulizi la bomu lililotokea mjini Mogadishu.

Akizungumza kutoka kibarazani kwake wakati wa ibada, Papa Francis alielezea namna alivyoguswa na tukio hili kwamba anaungana na familia zote katika kuwaombea majeruhi na wale waliopoteza maisha.

Bomu lililotegwa kwenye gari, lililipuka kwenye kituo cha ukaguzi chenye harakati nyingi katika mji mkuu wa Somalia jumamosi asubuhi kwa saa za huko.

Mamlaka ilieleza kuwa watu wengi waliofariki walikuwa wanafunzi wa chuo kikuu wanaorudi kwenye masomo pamoja na maafisa polisi.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed alilaani vikali shambulizi hili na kuliita kitendo cha ugaidi na alilishutumu kundi lenye msimamo mkali wa la Al Shabaab la nchini Somalia, ambalo lina uhusiano na al-Qaida ambao pia wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara yanayosababisha vifo kwenye majengo yenye maduka mengi ya biashara na mashule katika nchi jirani ya Kenya.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Mkamiti Juma Kibayasi, Washington, DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG