Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Maangamizi ya Rwanda (ICTR) Jumanne imewatia hatiani maafisa wanne waandamizi wa zamani wa jeshi la Rwanda, wakiwemo majenerali wawili kwa kuhusika kwao katika mauaji ya kimbari nchini mwao mwaka 1994.
Waliokutwa na hatia ni pamoja na aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Rwanda, Jenerali Augustin Bizimungu aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Jenerali Augustin Ndindiliyimana ambaye mahakama imeamua kwamba miaka 11 aliyokwisha tumikia tangu alipokamatwa, iwe ndiyo adhabu yake na hivyo kuamuru aachiwe huru.
Wote wawili walikutwa na hatia kwa mauaji ya maangamizi, uhalifu dhidi ya binadamu kwa kufanya mauaji, kuteketeza kizazi na kukiuka mkataba wa kimataifa wa Geneva juu ya haki za binadamu wakati wa vita lakini Jenerali Bizimungu pia amekutwa na hatia katika ubakaji uliofanywa na askari waliokuwa chini ya mamlaka yake.
Katika hukumu hiyo pia, Meja Froncois-Xavier Nzuwonemeye na Kapteni Innocent Sagahutu wametiwa hatiani kwa tuhuma za mauaji na ukiukwaji wa mkataba wa haki za binadamu wa Geneva wakati wa vita na kuhukumiwa vifungo vya miaka 20 jela kila moja.
Jaji Kiongozi wa Mahakama hiyo,Joseph Asoka de Silva alifafanua kwamba Meja Nzuwonemeye na Kapteni Sagahutu pamoja na mambo mengine walihusika na mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Rwanda wakati wa mauaji ya hayo, Agathe Uwingiliyimana na askari 10 wa Kibelgiji waliokuwa katika kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo (UNAMIR), Aprili 7, 1994.
‘’Mahakama imebaini kwamba Nzuwonemeye na Sagahutu waliamuru kufanyika kwa mauaji ya Waziri Mkuu Uwingiliyima’’ Jaji De Silva alitamka na kuongeza kwamba wote wawili pia wanahusika ‘’katika kosa la jinai kama viongozi wa Kikosi cha Upelelezi Jeshini kilichohusika katika mauaji ya askari wa UNAMIR, raia wa Ubelgiji.’’
Alipoulizwa muda mfupi baada ya kuachiwa huru kufuatia kukamilisha adhabu yake, Jenerali Ndindiliyimana hakuficha kusema ‘’nimefurahi sana sana kuachiwa huru baada ya miaka 11 ya kukaa ndani.’’Hata hivyo ingawa alikuwa bado na kiu ya kusema zaidi, alichukuliwa harakaharaka na maafisa usalama wa ICTR na kuondoka naye.