Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Oktoba 10, 2024 Local time: 22:14

Majaribio ya chanjo dhidi ya Corona yaanza Kenya


Kundi la kwanza la watu nchini Kenya wamejitolea kushiriki majaribio ya chanjo dhidi ya virusi vya corona iliyotengenezwa Uingereza.

Ni sehemu ya juhudi za kimataifa kupima ufanisi wa chanjo iliotengenezwa na chuo kikuu cha Oxford na kampuni ya kutengeneza dawa, Astra-zeneca.

Watu 14 waliojitolea, wengi wao wakiwa wafanyakazi wa afya, ndio wanashiriki kwenye jaribio la chanjo dhidi ya covid 19 nchini Kenya.

Awamu ya kwanza ya jaribio la chanjo hiyo inaongozwa na kituo cha utafiti KEMRI-Welcome Trust research program, kinachopatikana Kilifi.

Mmoja wa watafiti wa kituo hicho Dr Samuel Sang, anasema wanataka kuhakikisha kwamba chanjo hiyo ni salama kwa wanainchi wa Kenya.

“Chanjo zilizogunduliwa na kuwa na mafanikio na salama kwa baadhi ya raia, haimanishi kwamba itakua na mafanikio kwa raia wote wa dunia. Kwa hiyo kulikua umuhimu wa kutathmini iwapo chanjo hiyo ni salama na inafaa kwa wakenya waliojitolea, kuhakikisha wakenya wanajitolea kwa wingi kwa ajili ya jaribio la chanjo hiyo, lazima jaribio hilo liwe na mafanikio.” Amesema Dr. Sang

Kwa mjibu wa shirika la afya duniani (WHO), kuna karibu majaribio 100 ya chanjo dhidi ya covid 19 yanayofanywa kwa binadamu katika awamu ya kwanza.

Lakini wachambuzi wanasema, wakati utafiti wa chanjo unaendelea, kugawa kwa usawa chanjo hiyo wakati itapatikana bado ni changamoto.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni na kituo kiitwacho Duke Global Health Innovation, umeonyesha kwamba nchi zenye kipato cha juu zitapata kiurahisi chanjo hiyo ikipatikana.

Andrea Taylor ni kaimu mkurungezi wa mipango katika kituo cha Duke Global Health Innovation. Amesema kwamba “Matokeo yetu yanahitaji kueleweka katika mazingira ya uwezo mdogo wa utengenezaji. Nchi zenye kipato cha juu na cha kati tayari zimekwisha omba dozi billioni 3.8 hadi dozi billioni 5, hata kabla ya chanjo yoyote kuwekwa kwenye soko. Kwa hiyo, wakati majaribio kwa wanaojitolea yatakua yameidhinishwa, dozi ambazo zitatengenezwa katika mwaka wa kwanza au wa pili, zitakua tayari zimehifadhiwa kwa ajili ya nchi zenye kipato cha juu.”

Lakini Talyor anasema suala la kipato sio kikwazo.

“Uongozi kutoka nchi zenye mapato ya chini umebadilisha mjadala. Mfano, umoja wa Afrika na kituo chake cha kudhibiti magonjwa- Africa CDC, wanaratibu mkakati wa kiafrika wa kukusanya fedha kwa ununuzi wa chanjo na kuongeza ufadhili barani Afrika. Jitihada kama hizo zinafanyika pia katika kanda ya Amerika kusini.

Ushirikiano huu wa kikanda ni wa kufurahisha kweli na unaweza kuimarisha kipaji cha nchi za kipato cha chini na msimamo wao kwenye soko la kimataifa.”

Wizara ya afya ya Kenya imesema wa wengine 360 waliojitolea watashirikishwa kwenye jaribio la chanjo dhidi ya corona kwa binadamu, mara tuu uthabiti na usalama wa chanjo utakua umethibitishwa mnamo miezi 12 ijayo kwa kundi la kwanza la waliojitolea.

Imetayarishwa na Patrick Nduwimana, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG