Saba hao ni pamoja na: Majaji wa Mahakama Kuu Luka Kimaru Kiprotich, Lydia Awino Achode, John Mativo Mutinga, Abida Ali Aroni, Frederick Ochieng’ Andago, Ngenye Grace Wangui na wakili Paul Gachoka Mwaniki.
Baada ya zoezi hilo lililoongozwa na msajili mkuu wa mahakama Anne Amani katika Ikulu ya Nairobi, rais Uhuru Kenyatta amewataka majaji hao saba wapya wa Mahakama ya rufaa kutumikia taifa kwa uaminifu, uadilifu na bila woga wala mapendeleo.
“Mnapochukua viti vyenu kwenye mahakama, kumbukeni kuwa Wakenya wanatarajia mengi kutoka kwa idara ya mahakama kuliko hapo awali. Wakenya wanatamani mahakama inayotoa haki bila woga au upendeleo kwa njia ya haraka, inayofikika na thabiti,” amesema Kenyatta.
Kenyatta ahimiza uadilifu
Aidha, Kenyatta aliyekuwa akizungumza muda mfupi baada ya kushuhudia kuapishwa kwa majaji hao amewataka kulitumikia taifa kwa uadilifu na kwa njia inayofuatana na sheria za nchi.
"Wakenya wanatarajia uongozi ambao wameukabidhi kwa mahakama kutekelezwa kwa uadilifu mkubwa na kwa kuzingatia kanuni takatifu ya kuendeleza manufaa ya taifa," Rais Kenyatta ameongeza.
Mahakama za Kenya zimekuwa zikipitia ugumu wa kupunguza mrundiko wa kesi zinazohitaji usuluhishi wa kasi, urahisi na usahihi baada ya rais Kenyatta mwaka jana kuteua majaji 34 kati ya 40 waliopendekezwa na JSC mnamo Juni 2020.
Rais Kenyatta alighairi kuidhinisha uteuzi wa majaji sita ambao ni Professa Joel Ngugi, George Odunga, Weldon Korir, Aggrey Muchelule, hakimu mkuu wa mahakama kuu Evans Makori na Msajili wa mahakama hiyo Judith Omange kwa madai kuwa sita hao hawakupita vipimo vya uadilifu.
Tofauti na hapo awali, wakati huu, rais Kenyatta hakutaja masuala yoyote ya uadilifu kwa majaji walioteuliwa tume ya huduma hiyo ya mahakama.
Umuhimu wa uteuzi huo wa majaji zaidi
Jaji Mkuu Martha Karambu Koome, ambaye pia ni rais wa idara ya mahakama ya Kenya, baada ya kushuhudia kuapishwa huko ameeleza kufurahishwa na uteuzi huo na kuutaja kuwa muhimu kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani.
“Jumla ya majaji 41 wameapishwa kushika wadhifa huo tangu kuteuliwa kwangu katika Ofisi ya Jaji Mkuu Mei 2021, na hivyo kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Mahakama kukidhi matakwa ya haki ya watu,” ameeleza Jaji Koome kupitia msururu wa machapisho katika mtandao wake wa Twitter.
Kwa muda mrefu, Mahakama ya Rufaa ya Kisumu na Nyeri hazijakuwa zikifanya kazi kutokana na upungufu mkubwa wa majaji na uteuzi wa majaji wa ziada wa Rufaa umewezesha kufunguliwa kwa vituo hivi, ameongeza Jaji Mkuu Martha Koome.
JSC ilikuwa imeorodhesha jumla ya wagombeaji 31 wa nafasi ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa kutoka kwa jumla ya wagombeaji 68 katika zoezi lililoanza Juni tarehe 27 mwaka huu.
Idadi ya majaji katika mahakama ya rufaa haitoshi
Akitangaza orodha ya majaji hao waliochaguliwa na JSC, Jaji Mkuu Koome alieleza kuwa kuchaguliwa kwa saba hao kulitokana na mchakato wa uajiri uliofanyika kwa njia ya umakinifu kuangazia utendakazi wa wagombeaji walioonesha nia ya kujaza nafasi hizo kwa kuzingatia sifa zao, jinsia, usawa wa maeneo ya Kenya, uadilifu na maslahi ya umma, kujaza nafasi zilizotangazwa kupitia gazeti rasmi la serikali mnamo Machi tarehe 14, mwaka huu.
Kuapishwa kwa majaji hao kunaongeza idadi ya majaji katika mahakama hiyo ya nafasi ya pili nchini Kenya kufikia hadi 26. Sheria inataka idadi ya majaji wa mahakama ya rufaa kuwa 30.
Kabla ya kufanyika kwa mahojiano haya ya uajiri, shirika la Katiba Institute, lilikuwa limewasilisha maombi mahakamani kutaka JSC kutofanya mahojiano mengine kwa kushindwa kuhakikisha majaji sita walioorodheshwa katika orodha ya awali ya kuajiriwa wameteuliwa afisini na Rais Kenyatta, na kudai kuwa si vyema kuanzisha mchakato mwingine wa kuwaajiri majaji bila Kenyatta kutekeleza wajibu wake wa kisheria. Kesi ambayo mahakama ya rufaa iliitupilia mbali.
Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi