Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Oktoba 07, 2024 Local time: 12:11

Mahakama ya katiba Burundi yamuunga mkono Nkurunziza


Waandamanaji wa upinzani Bujumbura wakipinga hatua ya Rais Nkurunziza kuwania muhula wa tatu
Waandamanaji wa upinzani Bujumbura wakipinga hatua ya Rais Nkurunziza kuwania muhula wa tatu

Mahakama ya Katiba nchini Burundi imemruhusu Rais Piere Nkurunziza kuwania muhula wa tatu madarakani ambao umegubikwa na utata.

Mahakama hiyo ilisema Jumanne kwamba rais ataweza kuwania tena kiti hicho bila kukiuka katiba ya nchi inayosema “kurudia tena muhula wa urais kupitia kipengele cha moja kwa moja cha haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa kisiasa” inaruhusiwa.

Lakini naibu rais wa mahakama hiyo amepinga maamuzi hayo na kukimbilia nchini Rwanda. Sylvere Nimpagaritse aliwaambia waandishi wa habari kwamba dhana yake haimruhusu kutia saini maamuzi ambayo ni kinyume cha katiba.

Rais Pierre Nkurunziza
Rais Pierre Nkurunziza

Muhula wa kwanza wa bwana Nkurunziza kama Rais ulitokana na matokeo ya kura ya wabunge. Wafuasi wa rais wanasema bwana Nkurunziza amehudumu muhula mmoja pekee kama matokeo ya ushindi wa uchaguzi mkuu na anastahili kuwania muhula mwingine kulingana na misingi hiyo.

Wakosoaji wanasema bwana Nkurunziza anakiuka katiba na mkataba wa amani wa Arusha wa mwaka 2000 ambao ulisaidia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi.

Juhudi za rais za kuongeza muda wake madarakani zimechochea maandamano ya mitaani katika mji mkuu, Bujumbura na kusababisha mapambano na polisi na kupelekea vifo vya watu wasiopungua 12.

Makamu Rais, Prosper Bazombanza alisema Jumanne kwamba serikali ipo tayari kuwaachia mamia ya waandamanaji waliokamatwa zaidi ya siku 10 zilizopita kwa masharti kwamba maandamano yasitishwe.

Wakimbizi wa Burundi wakielekea nchi jirani ya Rwanda
Wakimbizi wa Burundi wakielekea nchi jirani ya Rwanda

Ghasia zimechochea kiasi cha warundi 24,000 kukimbilia nchi jirani ya Rwanda tangu ghasia hizo zilipoanza April 26. Maelfu zaidi wamekwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC.

Akizungumza huko nchini Kenya siku ya Jumatatu, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry alisema Marekani ina wasi wasi mkubwa kuhusu uamuzi uliochukuliwa na Rais wa Burundi ambao anasema unahusisha moja kwa moja katiba”.

XS
SM
MD
LG