Mahakama hiyo imewataka waliokuwa wagombea urais, wafuasi wao, mawakala, na tume ya uchaguzi na mipaka, kusita kuzungumzia kesi hiyo nje ya mahakama.
Katika taarifa iliyotiwa saini na jaji mkuu David Maraga pamoja na majaji wengine sita, mahakama hiyo ya juu imewataka raia kuheshimu sheria inayowakataza kuzungumzia masuala ambayo yanajadiliwa mahakamani, ili kuipa nafasi ya kufanya uamuzi wake.
Tangu muungano wa NASA kuwasilisha hoja yao mahakamani kufuatia kutangazwa kwa rais Uhuru Kenyatta kama mshindi wa uchaguzi huo wa tarehe 8 mwezi huu, viongozi wa kisiasa wa mrengo huo na hata wale wa mrengo wa Jubilee, wamekuwa wakitoa kauli kuhusu kesi hiyo katika mikutano ya hadhara.
Kawa mujibu wa gazeti la Daily Nation, majaji hao pia wamewaonya waandishi wa habari dhidi ya kuvunja sheria wakati wa utekelezaji wa kazi zao.