Mahakama hiyo imesema kuwa idadi ya majaji inayotosheleza kusikiliza shauri hilo haikuweza kufikiwa.
Tangazo hilo linaonyesha kuwa marejeo ya uchaguzi wa rais utaendelea kufanyika Alhamisi bila ya pingamizi lolote.
Dazeni ya wanawake wakiwa wamevalia skafu nyeupe waliandamana Jijini Nairobi Jumatano kuonyesha kuunga mkono kwao uchaguzi huo ambao umepangwa kufanyika pamoja na kuwepo na wasiwasi wa kuzuka kwa vurugu.
Wakati siku zikikaribia watu kupiga kura kumekuwepo na mapambano yaliyojikariri kati ya polisi na waandamanaji, lililopelekea serikali kupiga marufuku maandamano katika miji mikubwa nchini Kenya wiki iliyopita.
Uchaguzi utakaofanyika Alhamisi utakuwa jaribio la pili katika mwaka huu kumchagua rais. Mahakama ya Juu ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8 kwa kile ulichokiita ni “dosari na ukiukaji wa sheria” uliogubika upeperushaji wa matokeo.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambaye alijitoa katika kinyang’anyiro hicho, na kuwataka wafuasi wake kupinga kile kilichofahamika kama ni muendelezo wa dosari zilizoendelea kuwepo katika Tume ya Uchaguzi.
Raila Odinga amesema : “ Tumetangaza hakutakuwa na uchaguzi Octoba 26, kitachotokea ni kujitangaza kwa Jubilee na kufanya kura ya maoni na siyo uchaguzi halisi katika Jamhuri ya Kenya. Uchaguzi utafanyika pale tu patakapokuwa na mazingira yanayoruhusu uchaguzi huru na wa haki.
Wakati huohuo Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amewahakikishia wafuasi wake kutakuwa na usalama wa kutosha katika vituo vya kupiga kura, akiongeza kuwa wale wanaopanga kuleta vurugu au kusababisha uvunjifu wa amani au kutishia wanaotaka kupiga kura watakiona kile kitakacho watokea.