Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 06, 2024 Local time: 11:34

Tanzania kuipatia Kenya madaktari 500


Rais Uhuru Kenyatta na Rais John Magufuli
Rais Uhuru Kenyatta na Rais John Magufuli

Tanzania imekubali ombi la kuipatia Kenya madaktari 500 watakaosaidia nchi hiyo kukubaliana na tatizo la uhaba wa madaktari katika vituo vyake vya tiba hasa baada ya kutokea kwa mgomo wa madaktari nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais Dkt John Magufuli amekubali kutoa madaktari hao baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi wa Wizara ya Afya ya Kenya uliotumwa na Rais Uhuru Kenyatta, Jumamosi Ikulu ya Dar es Salaam.

Kiongozi wa ujumbe huo Waziri wa Afya wa Kenya Dkt Cleopa Mailu amemueleza Rais Magufuli kuwa baada ya kutokea mgomo wa madaktari pamoja na uamuzi wa nchi hiyo kugatua madaraka katika sekta ya afya, imebainika kuwa nchi hiyo ina upungufu mkubwa wa madaktari ambao hauwezi kumalizwa kwa kutegemea madaktari wanaosomeshwa nchini humo bali kupata madaktari kutoka nje.

Dkt Cleopa Mailu aliyeongozana na Gavana wa Kisumu Jack Ranguma amesema Kenya ipo tayari kuwalipa stahili zote madaktari 500 watakaotoka Tanzania ikiwa ni pamoja na mishahara na nyumba za kuishi.

Kwa upande wake Rais Magufuli amesema Tanzania imekubali ombi hilo kwa kuwa Kenya ni ndugu, jirani na rafiki wa kweli wa Tanzania na amemtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Ummy Mwalimu kuharakisha mchakato wa kuwapata madaktari hao ili wawahi kwenda Kenya kutekeleza jukumu hilo.

“Matatizo ya Kenya ni matatizo ya Tanzania, tutawapatia madaktari hao 500 ili wakatoe huduma ya matibabu kwa ndugu zetu waliopo Kenya, na kwa kuwa mmenihakikishia kuwa madaktari wangu mtawalipa mishahara inavyotakiwa, mtawapa nyumba za kuishi, na mtahakikisha wanafanya kazi katika mazingira mazuri na salama mimi sina tatizo na naamini mambo yatakwenda vizuri,” amesema Rais.

Nae Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania Ummy Mwalimu amesema wizara yake ipo tayari kutoa madaktari hao haraka iwezekanavyo kwa kuwa Tanzania inao madaktari wengi wazuri ambao wamemaliza masomo yao na hawajapata ajira, na wengine wamemaliza mikataba yao ya kazi na bado wana uwezo wa kufanya kazi.

“Vigezo vikubwa ambavyo tutaviangalia ni kwanza awe amemaliza mafunzo ya vitendo (Internship) na pili awe amesajiliwa na Baraza la Madaktari la Tanganyika, kwa hiyo leo hii tutatoa tangazo na tumefurahi sana kwa sababu tunao madaktari wa kutosha ndani ya nchi na tunaweza kuwapeleka Kenya,” amesema Ummy Mwalimu.

XS
SM
MD
LG