Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Julai 17, 2024 Local time: 20:23

Magufuli aapishwa kuwa rais mpya Tanzania


John Magufuli akiapishwa kama rais mpya wa Tanzania (REUTERS/Emmanuel Herman)
John Magufuli akiapishwa kama rais mpya wa Tanzania (REUTERS/Emmanuel Herman)

Mshindi wa uchaguzi wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ameapishwa Alhamisi kama rais mpya wa Tanzania katika sherehe zilizohudhuriwa na maelfu ya wananchi pamoja na marais sita wa Afrika.

Magufuli alishinda uchaguzi wa Oktoba 25 kwa kupata asilimia 58 za kura dhidi ya mpinzani wake mkuu Edward Lowassa ambaye alikuwa akiwakilisha muungano wa upinzani wa Ukawa.

Viongozi wote wa nchi za Afrika Mashariki - isipokuwa Pierre Nkurunzinza wa Burundi walihudhuria sherehe hizo mjini Dar es salaam. Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na Joseph Kabila wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo walikuwa miongoni mwa waliohudhuria.

Rais Mugabe wa Zimbabwe akimpongeza Rais Magufuli
Rais Mugabe wa Zimbabwe akimpongeza Rais Magufuli

​Rais Jakaya Kikwete anaondoka madarakani baada ya awamu mbili za miaka mitano mitano. Katiba inamzuia kiongozi aliyekaa madarakani kwa awamu mbili kugombania tena urais.

Tanzania sasa ina marais wastaafu watatu - Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Sherehe za Alhamisi mjini Dar es salaam zilisusiwa na viongozi wote wa upinzania wa umoja wa Ukawa. Sherehe hizo zimefanyika huku hatima ya matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar ikiwa bado haifahamiki.

Tume ya uchaguzi ya Zanzibar ZEC ilifuta matokeo ya uchaguzi siku mbili baada ya kura kupigwa kwa madai kuwa kulikuwa na matatizo mengi katika uchaguzi huo na kusema uchaguzi utarudiwa ndani ya siku 90. Chama kikuu cha upinzani CUF kimepinga hatua hiyo na kinaendelea kuishinikiza tume iendelee kuhesabu kura.

XS
SM
MD
LG