Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq anasema zaidi ya watu 12 wamefariki kufikia Jumatano usiku, katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko katika jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na Sauti ya Amerika, Bwana Sadiq amesema operesheni za uwokozi zinaendelea na wameanza kutoa msaada wa chakula kwa waathiriwa, huku vikosi vya usalama vimepelekwa kuhakikisha usalama na kulinda mali za watu.
Mfuriko hayo yalitokana na mvua nyingi zilizoanza Jumanne asubuhi na kuendelea hadi Jumatano usiku. Maelfu ya wakazi wamepoteza makazi yao na kulazimika kuhama maeneo ambayo nyumba zao zimefurika na maji.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Tanzania siku ya Jumatano inaeleza kwamba rais Jakaya Kikwete ametoa salamu zake za rambi rambi kupitia mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam akisema, "Ninakutumia wewe rambirambi zangu kutokana na vifo hivyo na kupitia kwako kwa familia, ndugu na jamaa walopoteza wapendwa wao katika balaa hili la mafuriko."