Wakaazi wa sehemu hiyo wameripoti milipuko mikubwa ya mabomu yanayorushwa na wanajeshi wa serikali dhidi ya waasi wa kundi la M23.
Ndege za kivita zimekuwa zikipaa mjini Goma, ambapo jeshi la serikali limeimarisha usalama kutokana na ripoti kwamba waasi wa M23 wanalenga kudhibithi mji huo muhimu wa kibiashara.
Maafisa wa usalama wamekuwa wakipiga doria katika mji wa Goma tangu jumapili usiku na kusajili vijana wanaojiunga na jeshi kwa ajili ya kupambana na waasi.
Waasi wa M23 wanaendelea kushikilia mji wa Bunagana, ulio kilomita 59 kutoka Goma. Waasi hao vile vile wanashikilia sehemu zingine ikiwemo Kiwanja, mji ulio kwenye barabara ya kutoka Bunagana hadi Goma.
Waasi wa M23, wakiongozwa na Bosco Ntaganda na Sultani Makenga, walidhibiti Goma mwaka 2012, baada ya wanajeshi wa serikali kukimbia na kuuwacha. Waasi hao waliondoka kufuatia shutuma za jumuiya ya kimataifa.
Jumla ya raia wa DRC 16,000 wamekimbilia Uganda kufuatia mapigano kati ya M23 na wanajeshi wa serikali ya DRC.