Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Februari 06, 2023 Local time: 03:34

Mbowe: Marehemu Macha alitumikia Chadema kwa dhati


Freeman Mbowe

Mjumbe wa Kamati Kuu wa CHADEMA na Mbunge wa Viti Maalum, Dkt Elly Macha ameaga dunia Ijumaa akiwa Uingereza kwenye matibabu.

Akitangaza msiba huo Ijumaa, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa nchini Tanzania, Freeman Mbowe amesema kuwa Dkt Macha alikuwa mmoja wa watu waliojitolea utaalam na taaluma zao kukitumikia chama hicho.

Marehemu amekuwa mstari wa mbele kuwatumikia watanzania tangu akiwa mwanachama wa kawaida, kabla hajawa Mjumbe wa Kamati Kuu na kisha Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema Mbowe.

"Msiba huu ni mojawapo ya pigo kubwa kwetu sisi CHADEMA na Watanzania wote kwa ujumla. Mama Macha alikuwa mtu aliyetoa muda wake, akitumia taaluma, utaalam na uzoefu wake kukishauri chama katika masuala mbalimbali. Amekuwa mstari wa mbele kabisa katika haki na masuala ya watu wenye ulemavu ndani ya chama na bungeni."

"Amefanya hivyo tangu akiwa mwanachama wa kawaida na akaendelea hata alipogombea na kuchaguliwa kuwa kiongozi wa ngazi ya juu kwa maana ya Mjumbe wa Kamati Kuu na baadae akawa mbunge. Kwa niaba ya Uongozi wa Chama natoa pole sana kwa familia, ndugu, marafiki wa marehemu pia kwa viongozi wa chama na wanachama wenzangu na wote walioguswa na msiba huu mkubwa. Tumuombee marehemu kwa Mungu amlaze marehemu pema," amesema Mbowe katika taarifa yake.

Marehemu Dkt. Macha aligombea na akachaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu katika uchaguzi mkuu wa ndani ya chama mwaka 2014 na mwaka 2015 alikuwa kati ya wagombea waliojitokeza kuwania uteuzi wa Ubunge wa Viti Maalum ambapo amekuwa mbunge mwenye mchango mkubwa bungeni na msemaji mkubwa wa masuala ya watu wenye ulemavu.

Taarifa za msiba, hususan ratiba ya kuwasili kwa mwili wa marehemu na mazishi, zitatolewa baada ya Familia, Chama na Ofisi ya Bunge kukamilisha taratibu zingine kadri inavyohitajika.

Wakati huo huo Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Y. Ndugai amesema amesikitishwa na kifo cha Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Dkt Elly Marko Macha.

Taarifa kutoka ofisi ya Mawasiliano ya Bunge inasema mpango wa kusafirisha mwili wa Marehemu kuja nchini ikiwa ni pamoja na taratibu za mazishi inaendelea kufanywa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Familia ya Marehemu.

Kufuatia msiba huu, Spika ameahirisha vikao vya kamati vilivyokuwa vinaendelea leo hadi kesho Jumamosi tarehe 1 Aprili, 2017.

Taarifa zaidi juu ya Msiba huu zitaendelea kutolewa na Ofisi ya Bunge kadri zitakavyopatikana.

XS
SM
MD
LG