Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Juni 05, 2023 Local time: 13:00

Maandamano ya mabadiliko Jordan na Misri yapamba moto


Waandamanaji wakipambana na askari huko Misri.

Maandamano ya wananchi yanaendelea katika nchi za Misri na Jordan katika harakati zinazozidi kupamba moto kudai mabadiliko ya kisiasa katika nchi hizo.

Maelfu ya waandamanaji wameingia katika mitaa ya Jordan wakitaka mabadiliko ya serikali na kujiuzulu kwa waziri mkuu Samir Al Rifai.

Huku wakiimba watu hao waliandamana katika mitaa ya mji mkuu wa Jordan Amman na miji mingine kadhaa.

Waunga mkono wa upinzani katika nchi hiyo wamefanya mfululizo wa maandamano katika wiki iliyopita sawa na yale ya Tunisia ambayo yalipelekea kuondolewa kwa rais wa nchi hiyo mwezi huu.

Wajordan wamekuwa wakidai nafuu katika bei ya vyakula na pia wanaishutumu serikali kwa kushindwa kupambana na rushwa.

Na huko Misri maelfu ya wamisri wamejazana katika mitaa ya nchi hiyo leo baada ya sala ya Ijumaa wakizidisha shinikizo kwenye maandamano wakidai kumalizika kwa utawala wa Hosni Mubarak wa miaka 30.

Ghasia ziliripotiwa huko Suez na Alexandria na maeneo mengine kadhaa ya Cairo. Shirika la habari la reuters limeripoti kuwa mwili wa mmoja wa waandamanaji hao ulibebwa katika mitaa ya Suez na waandamanaji wenye hasira.

Shirika la AP limeripoti kwamba mshindi wa tuzo ya Nobel na mwanaharakati wa Misri Mohamed El Baradei yuko kwenye kifungo cha nyumbani. Awali shirika hilo la habari lilisema maafisa wa Misri walimshambulia kwa mabomba ya maji El Baradei mkuu wa zamani wa nishati ya atomiki ambaye alirudi Misri kutoka Austria alhamisi akisema angependelea kuongoza vugu vugu la upinzani.

XS
SM
MD
LG