Huduma za treni zilisitishwa na baadhi ya shule kufungwa huku taka zikiwa zimerundikana mitaani, umeme ulikatwa huku vyama vya wafanyakazi vikiongeza shinikizo kwa serikali kuondoa sheria inayoongeza umri wa kustaafu kwa miaka miwili hadi miaka 64.
Moshi mwingi ulitanda hewani kutoka kwenye rundo la uchafu uliochomwa na kuzuia usafiri kwenye barabara kuu karibu na mji wa Toulouse, kaskazini magharibi mwa Ufaransa.
Msemaji wa mamlaka ya viwanja vya ndege mjini Paris amesema maandamano karibu na mlango wa kuingia kwenye uwanja wa huo wa Roissy hayataathiri safari za ndege.
Maandamano mengine yamepangwa kufanyika nchini kote baadaye mchana, huku maandamano mengine yakilenga pia ghala ya mafuta.
Rais Emmanuel Macron jana Jumatano alisema sheria hiyo ambayo serikali yake iliyopitisha wiki iliyopita bila kura ya bunge, itaanza kutekelezwa mwishoni mwa mwaka huu licha ya hasira kuongezeka nchini kote.