Maelfu ya watu wameandamana katika barabara za Moscow mji mkuu wa Russia na katika miji mingine kote nchini humo Jumamosi kupinga kile wanachodai ni wizi wa kura katika uchaguzi uliokipa ushindi chama tawala cha United Russia Party kinachoongozwa na Vladmir Putin.
Polisi wanaripoti kuwa watu elfu 20 walishiriki katika maandamano hayo katika uwanja wa Bolotnaya Square mjini Moscow na kando kando ya mto kutoka maeneo ya bunge lakini waandalizi wanasema waandamanaji walikuwa zaidi ya elfu 50.
Utawala wa Moscow ulikuwa umetoa kibali kwa waandamaanji elfu 30 kukusanyika mahala hapo. Maafisa wa ulinzi walipiga doria wakitumia helikopta, magari ya kijeshi na polisi wa kupambana na ghasia.
Maandamano sawa na hayo yalifanyika katika miji mingine kote nchini Russia ukiwemo mji wa bandari wa Vladivostok ambapo mamia ya watu walibeba mabango yakiwa na maandishi yaliyosema “panya lazima waondoke”.