Vijana waliokuwa wamefunika nyuso zao walichoma matairi pamoja na kufunga barabara kuu iliyoko karibu na bahari inayotoka katikati mwa Tripoli kuelekea kwenye vitongoji vya magharibi, wakati maafisa wa usalama wakitazama bila kuingilia kati.
Video zilizorushwa na baadhi ya vyombo vya habari zimeonyesha maandamano zaidi kwenye mji wa Beni Walid pamoja na ule wa bandari wa Mistara. Kundi la vijana linalojiita BELTRESS limesema kwamba limepanga maandamano zaidi mjini Tripoli.
Kundi hilo linaitisha uchaguzi pamoja na kuvunjwa kwa serikali mbili hasimu pamoja na mabunge tofauti yalioko. Hasira miongoni mwa wakazi zimechochewa na ukosefu wa umeme kwa hadi saa 18 kwa siku, wakati huu wa msimu wa joto, licha ya taifa hilo kuwa lenye utajiri mkubwa zaidi wa mafuta barani Afrika.
Taifa hilo limekumbwa na misukasuko ya kisiasa tangu mwaka wa 2011, baada ya muungano wa NATO kumuondoa madarakani na kumuua kiongozi wa muda mrefu Moamer Kadhafi.