Zimesalia saa chache Sudan Kusini ianze sherehe rasmi za uhuru wake na mji mkuu wake Juba unajiandaa kwa sherehe hizo Jumamosi Julai 9.Sherehe rasmi zitafanyiwa katika ukumbi wa John Garang, ukumbi uliopewa jina hilo kwa heshima ya mtu aliyeoongoza waasi wa Sudan Kusini wakati wa vita vya miaka 20 vya wenyewe kwa wenyewe. Mojawapo ya sherehe zinazosubiriwa zaidi na za mwanzo kabisa ni wimbo wa taifa utakaoimbwa kwa mara ya kwanza. Maneno yake yaliandikwa na wanafunzi wa chuo kikuu cha Juba, na yanaelezea matumaini, heshima kwa Mwenyezi Mungu na kumbukumbu kwa wote waliokufa wakati wa mtafaruku.Mamia ya wageni mashuhuri wa kimataifa watahudhuria sherehe hizo akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na hata rais wa Sudan Omar al-Bashir. Mwaliko wa Bw. Bashir lakini unazua hisia mbalimbali wengine wakimwona kama ishara ya ukandamizaji na kwa baadhi ya raia wa Sudan Kusini, wanasubiri kwa hamu na ghamu kumwona Bashir, pale bendera ya Sudan itakaposhushwa na bendera mpya yenye rangi sita ya Sudan Kusini kupaa na kupepea siku rasmi ya Uhuru wake Jumamosi.
Maandalizi ya uhuru wa Sudan Kusini

Raia wa Sudan Kusini wasubiri kwa hamu kuu sherehe za uhuru wao