Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 03, 2024 Local time: 17:00

Maafisa watano wa polisi wameuawa Mogadishu kwa bomu la kujitoa mhanga


Mlipuko wa bomu la kujitoa mhanga mjini Mogadishu, Somalia
Mlipuko wa bomu la kujitoa mhanga mjini Mogadishu, Somalia

Mlipuko huo ulisababishwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliyevalia vazi la kujilipua ambaye aliwaendea maafisa hao nje ya kituo cha wilaya ya Waberi majira ya saa tatu na nusu usiku kwa saa za huko, mashahidi walisema

Maafisa watano wa polisi ni miongoni mwa watu wasiopungua sita waliouawa Jumapili jioni na bomu la kujitoa mhanga mjini Mogadishu, mashahidi na maafisa walisema.

Meja Sadiq Aden Ali, msemaji wa jeshi la polisi la Somalia alithibitisha kwa vyombo vya Habari kuwa makamanda wawili wa polisi ni miongoni mwa waliouawa.

Meja Ahmed Abdullahi Bashane, kamanda wa wilaya ya Waberi huko Mogadishu na Meja Abdibasid Mohamud Agey, naibu kamanda wa zamani wa idara ya polisi ya Weliyow Adde, waliuawa pamoja na maafisa wengine watatu wa polisi. Raia mmoja ambaye alikuwa akiishi karibu na kituo hicho cha polisi pia aliuawa katika mlipuko huo.

Mlipuko huo ulisababishwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliyevalia vazi la kujilipua ambaye aliwaendea maafisa hao nje ya kituo cha wilaya ya Waberi majira ya saa tatu na nusu usiku kwa saa za huko, mashahidi walisema.

Watu sita wengine walijeruhiwa katika mlipuko huo, kulingana na taarifa ya polisi.

Shahidi ambaye hakuweza kutajwa jina lake kwa sababu za kiusalama alisema Bashane alikufa katika eneo la tukio wakati Agey alifariki kutokana na majeraha aliyopata baada ya kuondolewa kwenda sehemu nyingine kwa matibabu.

Masaa matatu kabla ya mlipuko huo, Bashane alituma ujumbe wa “Mother’s Day” akimtakia heri mama yake kwenye ukurasa wake wa Facebook.

XS
SM
MD
LG