Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 10, 2024 Local time: 19:02

Maafisa wa zimamoto wa Afrika Kusini wafariki dunia kwa moto


Maafisa wa zimamoto wa Afrika Kusini wakiwa katika harakati za kuuzima moto kwenye msitu wa karibu na Hanover Park, Cape Flats, mjini Cape Town, Afrika Kusini, Machi 11, 2024.
Maafisa wa zimamoto wa Afrika Kusini wakiwa katika harakati za kuuzima moto kwenye msitu wa karibu na Hanover Park, Cape Flats, mjini Cape Town, Afrika Kusini, Machi 11, 2024.

Maafisa sita wa kikosi cha zimamoto wamefariki dunia walipokuwa wakipambana na moto katika jimbo la KwaZulu-Natal mashariki mwa Afrika Kusini na wengine wawili wako katika hali mbaya kwa mujibu wa taarifa ya Jumatatu ya idara ya huduma za dharura.

Mamlaka zimesema zinashuku kuwa moto huo wa Jumapili huenda uliwashwa na wawindaji haramu wanaojaribu kuwanasa wanyama na kuwauwa.

Maafisa watatu wa kikosi cha zimamoto wamefariki dunia katika eneo la moto karibu na mji wa Boston, uliopo kilomita 130 kutoka pwani ya mashariki ya jiji la Durban, msemaji wa huduma za dharura Roland Robertson amesema.

Ameongeza kuwa maafisa wengine watatu walitibiwa na kuwekewa mashine za kupumulia, lakini wote walifariki dunia mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo.

Afisa mmoja bado yuko kwenye mashine ya kupumulia hospitalini, na mwingine pia yuko katika hali mbaya, amesema.

Robertson amesema baadhi ya majangili pia wanasadikiwa kujeruhiwa katika moto huo karibu na mashamba ya watu binafsi kutokana na upepo na ardhi kavu kuwafanya kuteketea bila kudhibitiwa. Hakuna ripoti za kukamatwa kwa washukiwa wa ujangili.

Moto wa msituni umewaka katika maeneo mengine ya KwaZulu-Natal wiki iliyopita kutokana na joto na upepo, ambao umesababisha vifo vya watu wengine saba katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, serikali ya eneo hilo imesema.

Moto huo umetokea wakati upande mwingine wa Afrika Kusini ukikumbwa na dhoruba nyingi, na kuleta upepo mkali na mafuriko. Mfululizo wa hali ya baridi kutoka Bahari ya Atlantiki iamesababisha uharibifu mkubwa mjini Cape Town na maeneo ya jirani katika ncha ya kusini magharibi mwa nchi kwa muda wa siku 10 zilizopita. Takriban watu 15,000 wameathirika na maelfu ya nyumba na majengo mengine yameharibiwa.

Forum

XS
SM
MD
LG