Uchaguzi wa mapema tayari unaendelea kwenye majimbo mengi ya Marekani, wakati mamilioni ya Wamarekani wakishiriki zoezi hilo moja kwa moja hapo Novemba 5. Jimbo la Kaskazini Magharibi mwa Marekani la Washington, limedhibitishia VOA Jumatatu kwamba polisi na maafisa wa FBI wanachunguza ripoti ya kuwepo kifaa cha kuwasha moto ndani ya sanduku la kura mjini Vancouver, Jumatatu.
Maafisa wamesema kuwa hakuna aliyejeruhiwa ingawa baadhi ya masanduku yaliharibika. Video iliorushwa na vyombo vya ndani vya habari imeonyesha wazima moto wakielekea kwenye eneo la tukio, wakati baadhi ya masanduku ya kura yakichomeka. Maafisa kutoka jimbo jirani la Oregon kwenye mji wa Portland pia waliripoti kuwa masanduku kadhaa yalishambuliwa kwa kifaa hicho, takriban nusu saa kabla ya tukio la Washington.
Mashambulizi ya masanduku ya kubebea kura Washington na Oregon yanafuatia mengine ya wiki iliopita huko Phoenix, Arizona Kusini Magharibi mwa Marekani. Maafisa walikamata mshukiwa mmoja kwa kuwasha moto sanduku la kubebea barua na kuharibu takriban kura 20. Matukio hayo yamefanyika wakati maafisa wa usalama wa Marekani wakionya kuhusu uwezekano wa mashambulizi wakati wa uchaguzi kutoka kwa magaidi waliopo nchini.
Forum