Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 10, 2024 Local time: 21:41

Lugha za asili zitumike kuboresha msamiati wa Kiswahili


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Philip Mpango katika maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Philip Mpango katika maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani

Lugha za asili barani Afrika ni vyema zitumike katika kuboresha msamiati wa Kiswahili ili kuendelea kukikuza na kutumika katika nyanja mbali mbali ikiwemo katika fani za sayansi na teknolojia.

Wataalamu wa lugha ya Kiswahili wameiambia VOA kuwa, lugha za asili zina ukaribu na muingiliano mzuri na Kiswahili kwa hiyo familia zitumie lugha hizo kukuza lugha ya Kiswahili ambayo inaendelea kukua na kubadilika.

Profesa Aldin Mutembei ambaye ni mwenyekiti wa kigoda cha uprofesa cha mwalimu Nyerere katika Kiswahili kwenye Chuo kikuu cha Dar es Salaam amesema Kiswahili hakikandamizwi na lugha za asili bali kinaboreshwa na kuendelezwa.

Amesema kuwa lugha za asili zinatumika kama “mizizi na kujenga msamiati wa Kiswahili, kwa kuwa “Kiswahili kina ukaribu na lugha za asili kuliko lugha za kigeni.”

Naye Tabia Ali, mwalimu wa lugha katika shule ya sekondari ya Zanaki, jijini Dar es Salaam amesema nchi kama Tanzania ambako Kiswahili kinatumika kama lugha kuu ya mawasiliano inayoyaunganisha makabila mengi, lugha za asili zitumike kuboresha misamiati iliyotokana na lugha hizo yakiwemo matamshi na matumizi ya maneno ili kuleta maana iliyokusudiwa.

Profesa na mkurugezi katika taasisi ya taaluma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Shani Omary, amewataka wazazi wazijue lugha zao za asili na wawaelimishe watoto kuhusu lugha hizo.

“Kama mmatumbi azungumze lugha yake ya kimatumbi, na kama mzaramo azungumze lugha yake ya kizaramo ili mtoto pale anapoanza kutumia lugha basi aweze kumfundisha lugha zote hizo” na kuongeza kuwa “mtoto anaweza kujifunza lugha nyingi kwa wakati mmoja.”

Alisema iwapo wazazi hawazijui lugha zao za asili inakuwa vigumu kwa mtoto kuzijua lugha hizo ambazo zina uwezo wa kuendeleza ukuaji wa Kiswahili.

Forum

XS
SM
MD
LG