Majaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu huko the Hague wameamrisha kuwa mtuhumiwa wake wa kwanza Thomas Lubanga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hata hivyo, Lubanga hataachiliwa katika siku tano zijazo wakati upande wa mashitaka unatafakari kukata rufaa.
Kesi dhidi ya Lubanga iliahirishwa wiki iliyopita baada ya majaji kusema kumetokea ukiukaji wa taratibu za uendeshaji kesi. Ukiukaji huo umetokea baada ya ofisi ya mwendesha mashitaka kushindwa kumtambulisha shahidi muhimu katika kesi hiyo. Lubanga alishitakiwa kwa kuandikisha watoto wadogo katika jeshi lake la uasi. Amekana mashitaka hayo.
Katika uamuzi wao majaji walisema "mshitakiwa hawezi kuwekwa kizuizini kwa misingi ya dhana tu, kwamba katika siku zijazo mashitaka yanaweza kufunguliwa tena."
Hata hivyo, upande wa waendesha mashitaka una siku tano kukata rufaa, na kama rufaa hiyo itakubalika Lubanga atabaki gerezani mpaka rufaa hiyo itakaposikilizwa, kulingana na taarifa ya ICC.
Lubanga alikuwa akiongoza kundi la wanamgambo wa kabila la wahema la UPC - moja ya makundi sita yaliyokuwa yakipigania eneo la Ituri lenye utajiri wa madini kati ya mwaka 1999 na 2003.