Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 30, 2022 Local time: 17:00

Wakili Fatma Karume asema, 'Lissu ni Mkatoliki si Mwislamu'


Tundu Lissu akiwa katika mikutano ya hadhara na wafuasi wa chama chake

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amefikishwa mahakamani Jumatatu kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimesema kuwa upande wa Serikali umedai kuwa maneno yake ni yenye kuleta chuki kwamba Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kidini, kikabila na kikanda.

Upande wa Jamhuri unawakilishwa na mawakili wanne akiwamo Paul Kadushi, Mutalemwa Kishenyi na Simon Wankyo wakati upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili 18 wakiwamo Fatma Karume na Pete Kibatala.

Akijibu hoja hiyo wakili wa upande wa utetezi, Fatma Karume alidai dhamana ni haki ya mshtakiwa na wala si haki ya Serikali wala mawakili wa Serikali.

“Napenda kuwakumbusha mawakili kwamba Lissu hapa hajahukumiwa, kwa maneno yao wenyewe mpaka sasa wanasema upelelezi haujakamilika, upelelezi haujakamilika halafu wanataka wewe utumie mamlaka yako kumuweka ndani.

“Wanataka mahakama imfunge Lissu, tukumbuke Mheshimiwa Lissu ni mpinzani na CCM ndio inawakilishwa, wanataka imfunge kwa sababu tu wameamua wao kuna meneno kasema ya uchochezi, kesi zote zilizopo hapa zimeletwa baada ya mwaka 2015 baada ya kuingia madarakani Magufuli.

“Ukitazama kesi nne hadi sasa hakuna hata moja waliyoikamilisha…wanasema tu kazi hawafanyi, wameshindwa hata moja na zote sababu Lissu kapaza sauti.

“Kila akipaza sauti wanaleta kesi kuimaliza wanashindwa, wanasema wanazuia dhamana eti kwa usalama wa mheshimiwa Lissu pia, hakuna anayetaka kumdhuru Lissu, Serikali ndio inataka kumdhuru sababu wamemshtaki mara sita.

“Wao ndio wanataka kumdhuru, hakuna mwananchi anayetaka kumdhuru… sisi hatutaki kumdhuru ila ni wao, Mheshimiwa Lissu ana haki ya kusema sio kuletwa hapa, wanasema analeta chuki za kidini…Lissu ni mkatoliki si Mwislamu.

“Kuna mambo kayaona hayaendi ndio kapaza sauti, sasa wanataka wamweke ndani kwa ridhaa yako mheshimiwa ili sauti yake isisikike.

“Kusema anyimwe dhamana kwa usalama wake…hiki ni kiini macho, wanajifanya wanampenda sana Lissu..eti akiwa nje ataharibikiwa,” alidai Karume na kuiomba mahakama impe dhamana mteja wake.

Awali Kishenyi akisoma hati ya mashtaka alidai mshtakiwa anakabiliwa na shtaka la kutoa lugha ya uchochezi Julai 17, mwaka huu maeneo ya Mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni

“Mheshimiwa hakimu mshtakiwa anadaiwa kusema kwamba Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini.

“Anadaiwa kusema vibali vya kazi vinatolewa kwa wamishionari wa kikatoliki tu huku madhehebu mengine yakiachwa kupanga foleni uhamiaji, viongozi wakuu wa Serikali wanachaguliwa kutoka kwenye familia, kabila na ukanda…….acheni woga pazeni sauti.

“Anadaiwa kusema kila mmoja ……tukawaambie wale ambao bado wanampa msaada wa pesa Magufuli na Serikali yake kama tulivyowaambia wakati wa Serilkali ya Makaburu.

“Anadaiwa kusema hii Serikali isusiwe na Jumuiya ya Kimataifa,isusiwe kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia kwa sababu ya utawala huu wa kibaguzi…..yeye ni dikteta uchwara,” alidai Kishenyi kwamba maneno hayo alitamka Lissu na kwamba yalikuwa na lengo la kuleta chuki.

“Kutokana na kujirudia kwa makosa ya kuleta chuki kwa jamii ya Watanzania ndio maana tunaomba mshtakiwa asipewe dhamana, haya matamshi yaliyosomwa mahakamani si ya kawaida, yanasababisha chuki baina ya Watanzania na madhara yake si madogo kama yataachwa na kunyamaziwa,”alidai na kuongeza kwamba asipewe dhamana kwa usalama wake pia, upande wa Jamhuri ulieleza hilo.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG