Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 17:40

Kesi ya Lema: Upande wa mashtaka wabadilisha mbinu


Godbless Lema mbunge wa Arusha wa chama cha Chadema akifikishwa mahakama kuu Arusha
Godbless Lema mbunge wa Arusha wa chama cha Chadema akifikishwa mahakama kuu Arusha

Mawakili wa mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya chama cha upinzani cha Chadema, Godbless Lema wamelalamika kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha hoja yao Mahkama Kuu huko Arusha, Tanzania.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya VOA, mmoja wa mawakili hao, Peter Kibatala amesema kuwa upande wa serikali badala yake umepeleka notisi mahakama kuu ya kukata rufaa ili kuendelea kuchelewesha utaratibu wa Lema kupewa dhamana.

"Tayari upande wa mashtaka wameshaona kwamba Mahakama Kuu inaelekea kusikiliza hoja ya ziada ambayo upande wetu ni kuwa mteja wetu kunyimwa dhamana na mahakama ya chini," alisema wakili huyo.

Wakili huyo alisema kuwa sasa kesi ambayo awali ilipangwa Januari 2 hivi sasa haitakuwepo na hivyo wanasubiri uamuzi wa mahakama kuu utakaotolewa Januari 4.

Wakili Kibatala alisema kuwa kama inavyojulikana mahakama ya rufani huwa haikutani kwa haraka na wakati mwingine inachukua mwaka mzima au miezi sit au minne, kitu ambacho kitamuacha mteja wetu akae jela kwa muda huo wote.

Godbless Lema mbunge wa Arusha akitoa hoja bungeni
Godbless Lema mbunge wa Arusha akitoa hoja bungeni

Mnano Novemba 11, hakimu mkazi alimpa Lema dhamana lakini kabla ya kutoa masharti ya dhamana hiyo, upande wa serikali ulitoa notisi ya kukata rufaa.

Lema anashtakiwa kwa kutumia lugha ya uchochea inayoweza kusababisha hali ya sintofahamu.

Hata hivyo wakili huyo alisema upande wa utetezi tayari wameshawasilisha hoja zao Ijumaa kama walivyotakiwa na mahakama kuu.

Katika hati ya maandishi yenye kuelezea hoja za upande wa Lema ambao VOA ulipokea nakala, inaeleza kuwa wamesikitishwa na kitendo cha serikali kutowasilisha hoja yao kuhusu ombi la kunyimwa dhamana Lema.

Katika waraka huo wameelezea kuwa kitendo cha upande wa serikali kutowasilisha hoja yao ya maandishi ni sawa na kutofika mahakamani, na hivyo hilo ni wazi kwamba linapelekea rufaa kutupiliwa mbali.

Mawakili wa mbunge huyo Jumatano walikubali rufaa ya serikali kuanza kusikilizwa kwa njia ya maandishi.

"Tumeona kuwa matokeo ya rufaa ni moja, rufaa ya Lema isimamishwe mpaka pale rufaa ya serikali itakapowasilishwa katika mahakama kuu, " alisema Bw. Kibatala.

Jaji wa mahakama kuu alitoa nafasi kwa pande zote mbili kuwasilisha hoja za ziada, na kuwa wao wataendelea kusimama pale pale kwamba wanapinga uamuzi wa mahakama hiyo ya chini kumnyima mteja wao dhamana.

XS
SM
MD
LG